Ripoti ya hali ya hewa barani Afrika ya mwaka 2022, inaonyesha kuwa kiwango cha ongezeko la joto barani Afrika kimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, huku hatari zinazohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi zikizidi kuwa mbaya.
Viongozi wa Afrika katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unaofanyika Dubai katika falme za kiarabu( COP28) wanasema ufadhili wa kukabiliana na hali ya hewa ni tone tu katika bahari ya kile kinachohitajika.
Takwimu zaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 110 katika bara Afrika waliaathiriwa moja kwa moja na hali ya hewa, na hatari zinazohusiana na maji mnamo 2022, na kusababisha zaidi ya dola bilioni 8.5 za uharibifu wa kiuchumi.
Viongozi wa Afrika Mashariki wanapaza sauti yao katika mkutano wa COP28.
Rais wa Kenya William Ruto amesema kukabiliana na mzozo wa hali ya hewa ni kazi ya dharura ambayo inahitaji juhudi za haraka na za pamoja.
"Ndio maana ni lazima tutetee hatua kali za hali ya hewa kwa kuweka malengo kabambe ya nishati mbadala na kutekeleza sera za kijani katika ngazi zote za utawala,"
Rais wa Tanzania Samia Suluhu alisema kuwa ahadi amabayo dunia iliweka Coppenhagen ya kutoa dola bilioni 100 kwa hatua ya mabadiliko ya hali ya hewa ingawa ni kidogo sana kuliko inavyotakiwa bado haijafika.
"Huko Paris tuliazimia kuweka ongezeko la joto chini ya nyuzijoto 1.5 hata hivyo kiwango cha ongezeko la joto sasa ni cha kutisha," Rais Suluhu aliambia mkutano wa COP28, " ni lazima kusemwe wazi kuwa ahadi ambazo hazijatekelezwa zinalegeza mshikamano na kuaminiana kwani kuna matokeo mabaya na ya gharama kubwa kwa nchi zinazoendelea."
"Nchi yangu inapoteza asilimia 2 hadi 3 ya pato la taifa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi," Rais Suluhu ameongezea, huku asisema kuwa wataalamu wanaonya kuwa mifumo ya kukumbana na tabia nchi zinazoonekana kutumiak hazileti mabadiliko ya haraka yanayohitajika.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliambia mkutano wa COP 28 kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanathibitika moja kwa moja nchini Somalia.
"Kwa sasa tunakabiliana na janga la kibinadamu lililosababishwa na mafuriko makubwa, yanayoathiri mamilioni ya watu. Mzunguko huu wa majanga ya hali ya hewa unahitaji hatua za haraka za kimataifa," alisema.
"Lengo letu ni kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 30 ifikapo 2030, tukitetea ufadhili wa haki wa hali ya hewa na utekelezaji wa fedha kutoka mfuko za hasara na uharibifu. Kwa pamoja, tunaweza kuunda mustakabali wa kijani na mzuri zaidi,"
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit alisema nchi yake pia inahitaji suluhisho ya haraka kwasababu watu wanaishi kwa athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
“Kwa miaka minne sasa, nchi yetu inakabiliwa na mafuriko, ukame, joto la juu kupita kiasi, na mifumo ya mvua isiyo ya kawaida. Mambo haya yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri vibaya maisha ya watu wetu watu waliokimbia makazi yao,” rais Salva Kiir aliambia mkutano huo.
"Hiyo inasababisha mizozo kati ya watu waliohamishwa na jamii zinazowapokea. Kwa hivyo, amani na usalama vinaathiriwa wazi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.," ameongezea, "tumekuja kwenye COP28 hii tukiwa na matumaini kwamba sisi, viongozi wa dunia, tutajitolea kutekeleza masharti ya Mkataba wa Paris."
Uganda nayo imesema kuwa hivi karibuni katika baadhi ya sehemu za nchi zimekumbwa na mafuriko ya maporomoko ya ardhi , ongezeko ya joto n ukame ilhali inachangia asili mia 0.01 ya uchafuzi wa hewa duniani.
" Hivi karibuni ni asili mia 10% tu ya fedha kwa ajili ya mabadiliko hali ya hewa zilifikia waathiriwa, hii halikubaliki," waziri mkuu wa Uganda Robinah Nabbanja aliambia mkutano wa COP28.
" Uganda kwa hivyo inaunga mbinu za ufadhili wa hali ya hewa ambapo angalau 70% ya rasilimali zinatengwa kwa hatua iliyobinafsishwa ya kukumbana na janga hili ili jamii zote zifikiwe na msaada."
Katika COP28 ya mwaka huu, Rwanda imesema itatoa wito wa kuchukua hatua kabambe zaidi kuhusu hali ya hewa, kuongeza maradufu ufadhili wa kukabiliana na hali hiyo .
Serikali ya Rwanda inasema rais Paul Kagame pia atafanya ushawishi kwa jamii ya kimataifa kuwaelezea kwa nini Rwanda ni mahali pazuri pa uwekezaji wa kijani.