Kenya imeondoa hitaji la visa kwa wageni wote wanaotembelea nchi hiyo.
Rais William Ruto alitoa tangazo hilo siku ya Jumanne wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Ruto alisema hatua hiyo itahimiza usafirishaji huru wa watu na bidhaa, na kufungua Kenya kwa fursa zaidi za kibiashara.
"Kuanzia Januari 2024, Kenya itakuwa nchi isiyo na visa. Haitahitajika tena kwa mtu yeyote, kutoka pembe yoyote ya dunia, kubeba mzigo wa kutuma maombi ya visa ili kuja Kenya," alisema rais Ruto.
Ruto alikuwa ametangaza mapema mwaka huu mpango wa Kenya wa kuondoa vizuizi vya viza kwa Waafrika wote kabla ya mwisho wa 2023.
Ameshabikia 'VISA free'
Sasa amepanua msamaha huo kwa ulimwengu wote katika tangazo lake lipya.
Kiongozi huyo wa Kenya amekuwa akizungumzia hitaji la kuondoa vizuizi vya visa kama sehemu ya utekelezaji wa eneo la biashara huria duniani.
Rwanda, Gambia, Ushelisheli na Benin ni nchi nyingine za Kiafrika zenye sera ya kutopata visa. Wanne hao, hata hivyo, waliongeza safari zisizo na visa kwa raia wa Afrika pekee.
Wasafiri kwenda Kenya wangekaa nchini kwa muda usiozidi siku 90 kwa matembezi, utalii, matibabu au biashara.
"Muda wa kukaa nchini Kenya huanza tarehe ya kuingia Kenya," Tume Kuu ya Kenya inasema.