Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amehakikishia Tanzania kuwa tume hiyo inasimama nayo wakati inakumbana na athari ya janga la mafuriko katika eneo la nchi hiyo.
"Mshikamano wetu mkubwa na rais Suluhu Samia, serikali na wananchi wa Tanzania wakikabiliwa na mafuriko makubwa katika mkoa wa Hanang ambayo yamesababisha vifo vya mamia, kuharibu maelfu ya nyumba, mashamba na makazi," Faki amesema katika ukurasa wake wa X.
"Hatua ya kimataifa inahitajika sasa," amesema akiashiria kuwa dunia inafaa kuweka jitihada zaidi kukumbana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo ndiyo chanzo ya mafuriko.
Mafuriko hayo yametokea huku nchi 180 zikikutana mjini Dubai, katika Falme za Kiarabu katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi, COP28.
Nchini Tanzania Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshuhudia kazi ya kusomba matope kwenye mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara, ikianza kwenye barabara kuu ya kutoka Babati hadi Singida.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo, Waziri Mkuu amesema idadi ya watu waliokufa katika maafa hayo imefikia 67 ambapo watoto wawili waliokuwa wamelazwa wameaga dunia.
"Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapa pole sana na sisi serikali tutaendelea kutekeleza maelekezo yake ya kuwahudumia na kurejesha hali ya utulivu," amehakikishia waathiriwa.
"Kazi inayofanyika sasa ni kuondoa tope lote ili tupate level ya zamani na watu waweze kuendelea na kazi zao. Tuna makamanda 1,265 wa vikosi vyetu vya ulinzi, na wako hapa katika maeneo tofauti," ameongezea.
Wataendelea kufanya kazi ili kuhakikisha tunarejesha mji wa Katesh katika hali ya kawaida. Malengo yetu ndani ya siku mbili hadi tatu hali ya kawaida irejee," ameongeza.
Amesema maagizo ya rais kuhusu kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wote yanazingatiwa, watu walioko kambini wanahudumiwa na kwamba iko timu ya wataalamu kutoka serikalini ambayo inafanya tathmini ya athari za maafa na mwishoni itatoa taarifa rasmi.
Mapema leo, Waziri Mkuu aliwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na kutembelea wodi ya watoto, wanaume na wanawake.
Pia alikutana na timu ya madaktari bingwa kutoka Dodoma na Arusha inayoongozwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ernest Ibenzi ambaye alisema timu yake ina watu 21 wakiwemo madaktari bingwa 12 ambapo sita wanatoka Dodoma na wengine sita wanatoka Arusha.
"Hawa tisa ni madaktari wasaidizi, wataalamu wa usingizi na wauguzi wa vyumba vya upasuaji," alisema.