Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametaka tahadhari zote za msingi zichukuliwe ili kuepusha kutokea kwa janga jengine la mlipuko wa magonjwa. Rais Samia ameyasema hayo pindi alipotembelea eneo Katesh ambapo ameshuhudia maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya udongo ambayo mpaka sasa yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 60, na wengine kujeruhiwa.
Wakati huo huo, rais Samia ametaka Wizara ya Nishati nchini humo kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa umeme wa dharura baada ya miundombinu muhimu kuharibika kutokana na maporomoko hayo.
Aidha rais Samia amesema, wahisani walioshiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira wa COP28, Dubai, wamechangia bilioni 2.5 kwa ajili ya janga hilo.
Mafuriko mazito yaliyotokea mwishoni mwa juma yamesababisha vifo vya Watanzania 76 mpaka sasa, huku kaya 1,150 zikiwa zimeathirika na watu 5,600. Pia kumekuwa na majeruhi zaidi ya 117 pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara, maji na umeme.