Wananchi wa kawaida wanataka kuhusishwa katika mijadala ya mabadiliko ya tabia nchi / Picha: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Mijadala kuhusu mabadilliko ya tabia nchi yamekuwa mingi sana duniani. Barani Afrika viongozi wa nchi na washikadau tofauti walikutana nchini Kenya, mwezi Septemba kulijadili swala hili kwa kina na kutoka na muafaka.

Afrika inatafuta suluhu kwa changamoto hii ambayo inatishia maisha ya watu.

Lakini mijadala mingi imekuwa katika majukwaa ya viongozi na mashirika makubwa.

TRT Afrika iliingia mitaani na kuongea na wananchi kuona ni kwa kiasi gani wanajua kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Sauti za Wakulima

Sidi Otieno ni mkulima mdogo katika maeneo ya Migori kaskazini magharibi mwa Kenya . Anasema wakulima kama yeye wanaona athari ya mabadiliko ya tabia nchi kila siku.

"Tunaumia sana kama wakulima kwasababu mvua inanyesha na wakulima wanalima, lakini mvua inanyesha mno na kuharibu mimea na pia mvua ikiacha, kiangazi inakuja kwa nguvu zaidi." Sidi aansema.

"Zamani kidogo tulikuwa tunajua kwamba ikifika mwezi wa nne mvua inanyesha watu wanalima, lakini siku hizi inaweza ikafika muda mvua inanyesha mwezi wa tano, ama isinyeshe kabisa, na hii inaathiri mimea kama mahindi ambayo inachukua muda mrefu kupanda na kuvuna," Otieno anaelezea.

Wananchi wa kawaida wanasema wanataka kujumulishwa kwa mijadala ya mabadiloko ya tabia nchi /Picha: TRT Afrika

Franklin Okinya Obonyo, mkulima mwenzake anaiona mabadiliko ya tabia nchi kwa njia tofauti.

"Tunaathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi kwasababu tunatumia mbegu ambazo si za kiasili," anelezea Obonyo. " Hii inafanya mazao yetu kuzalishwa mara moja tu."

"Hatuwezi kuwa na lishe ya kutosha tukitumia mbegu za kemikali kwasababu haziwezi kupandwa tena, hii inatufanya tusizalishe chakula cha kutosha, mbegu za kemikali haziwezi kustahimili mabadiliko kali ya jua na mvua," Obonyo anaongezea.

Mabadiliko ya tabia nchi si kwa wakulima tu

Vijana nao wanaiona mabadiliko ya tabia nchi hasa mijini wanapoishi.

"Mimi nikisikia mabadiliko ya tabia nchi ninawaza kuhusu ukuaji wa miji," Dereva Mutua anealezea.

"Juhudi za serikali zetu kuboresha nchi kwa kujenga miji imepelekea kuaharibika kwa mazingira yetu na cha kusikitisha ni kuwa viongoizi wetu nia kama hawaelewi mathara wanayofanya," Mutua anaelezea.

Anaelezea kuwa ukuaji wa miji inapelekea miti kukatwa kwa ajili ya majumba kujengwa, viwanda vikijengwa kwa ajili ya maendeleo vinaongeza hewa chafu hewani na hatimaye hali ya hewa inaathirika.

Wale ambao hawapati nafasi katika majukwa makubwa wanatumia mbinu tofauti kupaza saudi dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi /picha: TRT Afrika

Fredrick Odhiambo, msanii mwenzake ambaye pia hufanya michoro aina tofauti anasema kwake, mabadilko ya tabia nchi inaangazia maendeleo ambayo nchi tofauti zinatafuta, bila kuwafunza wananchi wao jinsi ya kufanya juhudi za kutoharibu mazingira.

Mabadilko ya tabia nchi lazima iambatane na hali

Rachel Mwikali mtetezi wa haki za akina mama katika eneo ala makazi duni ya Mathare jijini Nairobi, nchini Kenya, anahusisha mabadilko ya tabia nchi na haki za binadamu.

" Hatuwezi kuongelea mabadilko ya tabia nchi bila kuongea kuhusu haki za binadamu hasa wanawake," Mwilkali anasema,

"Katika mijadala mingi ya mabadiliko ya tabia nchi , sauti za wanawake hazisikiki sana, ilhali wanaathiriwa sana, Chukua mfano wa hali ya maisha sasa ambapo kupata chakula imekuwa vigumu kwasababu hali ya hewa inaathiri uzalishaji wa chakula," Mwikali anaelezea zaidi.

" Hii inaleta vita manyumbani , kwasababu mwanaume ambaye ni kiongozi wa familia akikosa kuleta chakula cha kutosha , mwanamke alalamike , inapelekea vita vya hapa na pale manyumbani, Tunajionea visa vingi kama hivi katika vitongoji duni," Mwikali anasema.

Wananchi wanajua suluhisho

Viongozi wa Afrika na wataalamu wamependekeza suluhisho tofauti kuhusu jinsi ya kujikwamua kutoka kwa mabadiliko ya tabia nchi, lakini wananchi wa kawaida wana maoni yao pia.

Wasanii wametumia jukwa lao kuwapa sauti wananchi wa kawaida kutoa ujumbe kuhusu mabadiloko ya tabia nchi/ Picha: TRT Afrika

"Viongozi wakifanya mikutano mikubwa mikubwa ni lazima watulete sisi wananchi wa kawaida nasi tuelezee jinsi mabadiliko ya hewa inavyo tuathiri, "Otieno ambaye ni mkulima anasema.

"Maazimio mengi yanafanywa bila sisi kuulizwa maoni yetu ni gani, hatuskii wakitaja vile msaada utafikia watu mashinani na katika vitongoji duni kama yetu," Mwikali anasema, "ni nani atatetea akina mama katika kampeni ya mabadiliko ya tabia nchi?"

Nao vijana wanapendekeza kuwe na uelewa zaidi wa swala hili.

"Vijana wengi hata hawaelewi mabadiliko ya tabianchi ni nini, wanafikiri ni swala la wale waliosoma sana," dereva anaelezea.

"Serikali zetu ni lazima ziongeze uelewa wa jambo hili kwani tunapoelekea inaoneka kila mtu lazima ajitete vile atakavyojikwamua na mabadiliko ya hali ya hewa."

TRT Afrika