Eudes Ssekyondwa
TRT Afrika, Magharibi mwa Uganda
Wakimbizi katika kambi ya Nakivale, Magharibi mwa Uganda wanategemea sana shughuli za kilimo kwa ajili ya kujikimu kimaisha pamoja na familia zao.
Livingstone Matata, ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na amekuwa katika kambi hiyo kwa muda wa miezi mitatu pekee, lakini anasema, athari za mabadiliko ya tabia nchi zimekwamisha jitihada zao za kufanya kilimo endelevu.
“Tulipofika hapa Julai kuliwa na mvua kidogo, wenyeji wametuambia kuwa mvua ilipungua kutokana na ukataji miti uliokithiri,'' ameambia TRT Afrika. ''Mlima mzima ulifunikwa na miti lakini hali imebadilika kwa sasa, mazao yangu yote yamekauka,” anasema Matata.
Mkimbizi mwingine ni Bwiiza Mutonore ambae ni mama wa mtoto mmoja. Naye pia ni miongoni mwa waliotoroka kutoka DRC.
Anasema lengo lake ni kumlea mwanae, huku akitegemea kuni kama chanzo chake kikubwa cha kupika.
Hata hivyo, upatikanaji wa kuni ni kizungumkuti. Kila siku, analazimika kutembea kilomita kadhaa wa ajili ya kutafuta kuni, ambazo hazikidhi mahitaji yake yote ya siku.
"Ni shida kupata kuni za kupika, wakati mwingine wamiliki wa mashamba madogo wanatufukuza. Na kama hutapata kuni unaweza kulala bila kula," Mutonore anasimulia.
Kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi wanaohitaji kuni kwa shughuli za kila siku, kumechangia ukataji miti katika eneo hilo, hivyo, kuongeza athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo uhaba wa mvua.
Nyumbani kwa wakimbizi barani Afrika
Afrika inahifadhi zaidi ya asilimia 30 ya wakimbizi duniani kote, na Uganda inachukua nafasi kubwa katika kuwahifadhi wakimbizi.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, hadi mwishoni wa Septemba 2023, Uganda imeweza kuhifadhi zaidi ya wakimbizi 1,520,966 huku wanaotafuta hifadhi wakifikia 47,271.
Wanaoongoza orodha hiyo ni wakimbizi kutoka Sudan Kusini ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakimbizi wengine ni wale kutoka Somalia, Burundi, Eritrea, Rwanda, Ethiopia na Sudan. Idadi hii kubwa imechangiwa na sera rafiki za Uganda kwa wakimbizi. Miongoni mwa sera hizo, ni pamoja na kuwaruhusu wakimbizi kuendelea na shughuli zao za kila siku ikiwemo kilimo.
Lakini kuwahudumia kunazidi kuwa kugumu, hii ni kutokana na uhaba wa rasilimali hasa kutoka kwa mashirika ya misaada yanayotoa huduma za kibinadamu.
Kwa mfano, Shirika la Chakula Duniani, WFP lilipunguza mgao wa chakula kwa kila mkimbizi kutoka asilimia 70 hadi 60 kuanzia mwezi Aprili 2020.
Na imebaki asilimia 60 kutoka Februari 2021.
Kwa mfano, WFP ilihitaji kutumia dola senti 0.68 kwa kila mtu kwa siku, mwaka 2022 lakini kutokana na ufinyu wa rasilimali, hivi sasa inatumia dola senti 0.35 pekee kwa mtu mmoja kuhudumia wakimbizi.
Hii ni moja wapo ya sababu kuu, inayowasukuma wakimbizi kujiingiza katika shughuli za kilimo, kwa sababu chakula wanachopewa, hakiwatoshi.
"Wakimbizi wote wanaokaa hapa pamoja na msaada tunaowapa wanategemea zaidi ardhi kwa kilimo," anasema Santo Asiimwe, afisa mipango kutoka shirika la WFP katika makazi ya wakimbizi ya Nakivale.
"Hali ya hewa ni mbaya sana. Tunakaribia Oktoba na hakuna mvua," anasema.
Sera ya mlango wazi
Uganda inawapa wakimbizi haki ya kufanya kazi na uhuru wa kutembea kupitia kile inachokiita "mfumo wa kujitegemea."
Mtindo huo umesifiwa sana kuwa mojawapo ya sera mzuri na wezeshi kwa wakimbizi duniani.
Na hivyo ndivyo wakimbizi kama Matata na Bwiiza wanavyoweza kukidhi baadhi ya mahitaji ambayo wasiopata kutoka WFP.
"Kuweza kupata mahali pa kuishi ni muhimu sana kwetu, kama hatungeweza kujisaidia zaidi hata kwa kilimo, tungekumbana na njaa kali," Matata anasema. "Lakini sasa wakimbizi wengi wamekuwa wakikata miti kwa matumizi ya kuni au kwa ajili ya kilimo, na hilo ndilo linalotuathiri sasa,”
Baadhi ya wakimbizi wanaelewa vizuri sana athari za kukata miti lakini wanasema hawana namna nyengine zaidi ya kufanya hivyo.
"Watoto wangu wananiambia kila siku kuwa kuni hizi tunazotumia ndio chanzo cha mabadiliko ya hali ya hewa, kwamba inachangia sisi kutokuwa na mvua ya kutosha, lakini bila hiyo, tutapika vipi?" anauliza.
"Tayari sisi ni wakimbizi ambao hatuna chaguo hata kwa ajili ya kuishi," anasema.
Miti ni muhimu kwa sababu huondoa hewa chafu ya 'carbondioxide' kutoka katika hewa. Ina kazi ya kuhifadhi uasili unayohitajika kuhifadhi kaboni na kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa.
Matumaini ya kijani
Enoch Twagirayesu, ni mkimbizi kutoka Burundi, tofauti na wengine, yeye ameamua kuchukua hatua na kuwa shehemu ya mabadiliko. Ameanza kuhamasisha wakimbizi wenzake kurejesha kijani katika eneo hilo.
Hadi sasa wamepanda miti zaidi ya 350,000 ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
"Ndoto yangu ni kufanya makazi ya wakimbizi ya Nakivale kuwa ya kijani, sasa tunawahamasisha wakimbizi na jumuia zinazowapokea kupanda miti ndani ya mashamba yao ya migomba ya ndizi," anasema.
Twagirayesu anasema baadhi ya nyakati anatumia nguvu za ziada kutoa elimu ya umuhimu wa kupanda miti, zoezi ambalo wakati mwengine linaonekana gumu kutoka na baadhi kuamini kwamba, hayo sio makazi yao ya kudumu.
"Ni vigumu kuhimiza hasa vijana kuzoea utamaduni wa kupanda miti," anasema, "Kumbuka watu wengi wanawaza jinsi ya kuondoka kambini na kurejea maisha yao ya kawaida, hawataki kuwa wakimbizi milele."
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, ameipatia kandarasi taasisi ya kijamii inayoitwa Nsamizi Institute for Social Development ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo hilo kwa kupanda miti mingi zaidi.
Kuanzia Mei 2022 hadi 2026, walianzisha mradi ambao huwaongezea kipato wakimbizi kwa kulipwa pindi wanapoanda mbegu na kutunza miti.
Lengo lake ni kukuza miti ili kufufua maliasili inayokaribia kutoweka na kuwapa wakimbizi maisha endelevu.
"Tunapanda miti kulingana na malengo ya mwaka. Mwaka huu, tumelenga kupanda hekta 80 katika makazi ya Nakivale pekee na hekta 10 katika makazi ya Uruchinga," anasema Racheal Akamumpa, Afisa Nishati katika Taasisi ya Nsamizi ya Maendeleo ya Jamii.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa na washirika wake wanatumai kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo watakuwa wamebadilisha athari za mabadiliko ya tabia nchi katika eneo hilo, lakini pia kuchangia katika kupunguza kiwango cha kaboni nchini Uganda.
Twagirayesu anasema, matamanio ya kila mkimbizi ni kuweza kurudi nyumbani hivi karibuni, na ana matumaini kuwa mradi huu utaigwa na wengine.