Kulingana na matokeo ya awali yaliyochapishwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa hilo la Afrika Magharibi siku ya Jumapili, Rais wa Liberia George Weah na kiongozi wa upinzani Joseph Boakai wanakaribiana katika kinyang'anyiro cha uchaguzi cha urais wa Oktoba 10.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Liberia, NEC, imehesabu takriban asilimia 72.9% ya kura ya zaidi ya watu milioni 2.4 zilizopigwa kwenye vituo 5,890 vya kupigia kura, huku vikionyesha rais George Weah akiwa amepata asilimia 43.80 naye mpinzani wake Boakai akiwa amepokea asilimia 43.54%.
Joseph Boakai, mwenye umri wa miaka 78, anawania kiti hicho cha urais kwa mara ya pili baada ya kupoteza dhidi ya Weah kwenye raundi ya pili ya uchaguzi mnamo 2017.
Boakai pia ni makamu wa rais wa zamani wa Liberia.
Ili kuepuka uchaguzi huo kuingia raundi ya pili, mshindi lazima apate zaidi ya asilimia 50% ya kura zilizopigwa.
Weah, mwenye umri wa miaka 57, ambaye pia ni mwanasoka mstaafu aliyegeuka mwanasiasa, aliibuka mshindi katika raundi ya pili wakati wa uchaguzi wa mwaka 2017 akipata asilimia 61.5 ya kura naye mpinzani wake Boakai akizoa asilimia 38.5 ya kura.