Weah, ambaye alilelewa katika mitaa ya Monrovia, ni mwafrika pekee kushinda tuzo ya kifahari zaidi, Ballon D'or. Picha: Getty

Mamilioni ya raia wa Liberia walipiga kura Jumanne katika duru ya pili ya uchaguzi kati ya Rais George Weah na aliyekuwa makamu wa rais wa zamani Joseph Boakai.

Uchaguzi huo umeshuhudia ushindani mkali wa karibu kati ya wapinzani hao wawili wa zamani, na kurudisha kumbukumbu ya uchaguzi wa 2017 kati yao ambapo Weah alishinda kwa zaidi ya asilimia 61.

Katika duru ya kwanza ya kura zilizopigwa Oktoba 10, Weah, 57, ambaye aliingia madarakani mwaka 2018, na mwanasiasa mkongwe Boakai, 78, walikaribiana sana.

Ingawa Weah alishinda raundi ya kwanza kwa zaidi ya asilimia 43, na kuongoza kwa kura 7,126, hakufikia asilimia 50% iliyohitajika kupata ushindi wa moja kwa moja.

Awali, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki amewataka Raia wote wa Liberia kupiga kura kwa amani katika uchaguzi huo wa pili wa Urais nchini Liberia.

Mamilioni ya raia wa Liberia walipiga kura Jumanne katika duru ya pili ya uchaguzi kati ya Rais George Weah na aliyekuwa makamu wa rais wa zamani Joseph Boakai.

Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kwanza tangu Umoja wa Mataifa ulipomaliza kazi yake ya kulinda amani nchini Liberia mwaka 2018.

Kikosi hicho kiliundwa baada ya zaidi ya watu 250,000 kufa katika vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1989 na 2003.

Waangalizi wanasisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kukubali matokeo ya mwisho.

Zaidi ya watu milioni 2.4 wamejisajili kupiga kura.

Waliberia watachagua kati ya Weah, ambaye ni maarufu miongoni mwa vijana na Boakai, makamu wa zamani wa rais chini ya aliyekuwa rais Ellen Johnson Sirleaf, rais wa kwanza wa kike Barani Afrika.

Tume ya uchaguzi ina siku 15 kuchapisha matokeo lakini inaweza kutangaza mapema, mmoja wa maafisa wake, Samuel Cole, alisema.

Vurugu vya wakati wa kampeni vilisababisha maafa na hofu ya kutokea machafuko baada ya uchaguzi.

AFP