Uchaguzi wa urais wa Liberia unaonekana kuwa na uwezekano wa kuingia katika duru ya pili baada ya matokeo ya siku ya Jumatatu kuonyesha kuwa rais George Weah na kiongozi wa upinzani ambaye pia ni makamu wa rais wa zamani Joseph Boakai, wakikaribiana katika mbio za kura za urais kufuatia uchaguzi wa Oktoba 10.
Hii inamaanisha kuwa, raia wa Liberia watarudi tena kupiga kura na kumfanya nyota wa soka wa zamani Weah, aliye na umri wa miaka 57, wa chama cha muungano wa mabadiliko ya kidemokrasia (CDC), kushindana tena na Boakai, mwenye umri wa miaka 78, wa chama cha Unity Party (UP), kwenye duru nyingine ya pili kama ilivyotokea mnamo 2017.
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Liberia, yanaonyesha kuwa Boakai anaongoza kwa asilimia 43.70 ya kura, huku Weah akiwa na asilimia 43.65, hii ikiwa ni sawa na matokeo ya jumla ya asilimia 92.8 ya kura zilizohesabiwa kutoka vituo ya kupiga kura.
Boakai, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo chini ya rais wa zamani Ellen Johnson Sirleaf, anaongoza uchaguzi huo kwa kura 748,463, ambazo ni sawa 43.70%, akifuatiwa kwa karibu na Weah aliyepata kura 747,578, ambazo ni sawa 43.65%.
Kufikia sasa, hakuna aliyepata zaidi ya 50% ya kura zilizopigwa ili kuliepusha taifa hilo la Afrika Magharibi kuingia duru ya pili ya uchaguzi.