Jacob Zuma./Picha: AA

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameionya tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kutokuingilia masuala ya kisiasa, na badala kuitaka tume hiyo kuhakikisha kunakuwepo uchaguzi wa huru na haki.

Zuma alitoa kauli hiyo siku ya Jumatatu wakati akiwahutubia mamia ya wafuasi wa chama cha uMkhonto weSizwe (MK) nje ya Mahakama Kuu ya jimbo la Gauteng Kusini, ambapo chama chake kinachuana na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo (IEC) kuhusu uhalali wake kushiriki na kugombea katika uchaguzi utakaofanyika Mei 29.

Zuma, mwenye umri wa miaka 81, alisema kuwa tume hiyo haipaswi kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa, na kuongeza, “Chama kitakachoshinda kitakaa chini na vyama vingine ndani ya bunge na kukubaliana nani awe Rais, na sio tume ya IEC. Hili linashtua sana,” limeripoti shirika la habari la nchi hiyo (SABC).

Zuma pia amesisitiza kuwa bado ana haki ya kugombea nafasi ya Urais tena kama atapata ridhaa ya watu wa Afrika Kusini, akisema kuwa hakukamilisha mihula miwili ya utawala wake.

“Hakuna atakayenizuia kama nikiamua kugombea tena. Niliondolewa madarakani kabla ya kuisha kwa muda wangu,” aliwaambia waandishi wa habari.

Siku ya Jumanne, kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini alikata rufaa dhidi ya maamuzi ya maofisa wa uchaguzi waliomzuia kugombea kwenye uchaguzi ujao, huku shinikizo zaidi likiongezeka kuelekea mchakato huo.

Wiki iliyopita, tume ya uchaguzi iliondoa jina la mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye anakiunga mkono chama kipya cha upinzani, kwa kudharau maamuzi ya mahakama ya mwaka 2021.

Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mnamo Juni 2021 baada ya kukataa kutoa ushahidi mbele ya jopo lililokuwa likichunguza ufisadi wa kifedha wakati wa utawala wake.

Aliachiliwa huru kwa ajili ya matibabu, miezi miwili tu baada ya muda wake.

Tume ya uchaguzi ilisema hana sifa za kugombea mwezi Mei kwa sababu, kwani, kwa mujibu wa katiba, "mtu yeyote ambaye alipatikana na hatia kwa kosa na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 bila chaguo la faini" hawezi kugombea katika uchaguzi.

Wakiwa nje ya Mahakama hiyo, wanachama wa chama cha MK walionesha imani kuwa Zuma atashinda katika kesi hiyo.

Mahakama hiyo ya Uchaguzi inatarajiwa kutoa uamuzi sio tu kwa kesi ya chama cha MK, lakini kwa rufaa zingine tano ambazo ziliwasilishwa mbele yake siku ya Jumanne.

TRT Afrika