Paul Kagame wa Rwanda anakaribia kutwaa muhula wa nne kama rais. / Picha: AA

Rais wa Rwanda Paul Kagame amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi ambao utaongeza muda wa utawala wake kwa miaka mingine mitano, kulingana na sehemu ya matokeo yaliyotolewa Jumatatu.

Kama kiongozi mkuu tangu mwisho wa mauaji ya kimbari ya 1994 na rais tangu 2000, Kagame alipata 99.15% ya kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza baada ya 79% ya kura kuhesabiwa.

Ni zaidi ya 98.79% ya kura alizoshinda katika uchaguzi uliopita wa 2017 na kumweka mbele ya wagombea wawili pekee walioidhinishwa kushindana naye.

Mgombea wa chama cha Democratic Green Party Frank Habineza alipata 0.53% ya kura na Philippe Mpayimana wa kujitegemea 0.32%.

Matokeo ya kura ya Jumatatu hayakuwa ya kushangaza kamwe, huku utawala wa Kagame ukishutumiwa kuzima upinzani wa kisiasa, na wakosoaji kadhaa mashuhuri walizuiwa kugombea.

Mara tu baada ya matokeo hayo kutangazwa na kumpa Kagame muhula wa nne, aliwashukuru Wanyarwanda katika hotuba yake kutoka makao makuu ya chama tawala cha Rwandan Patriotic Front (RPF).

“Matokeo yaliyotolewa yanaonyesha alama nyingi sana, hizi si takwimu tu, hata ingekuwa asilimia 100, hizi si namba tu,” alisema.

"Takwimu hizi zinaonyesha uaminifu, na hilo ndilo muhimu zaidi," aliongeza. "Nina matumaini kwamba kwa pamoja tunaweza kutatua matatizo yote."

Kumiminiwa sifa

Matokeo kamili ya muda yanatarajiwa kufikia Julai 20 na matokeo mahususi ifikapo Julai 27.

Huku 65% ya watu wakiwa na umri wa chini ya miaka 30, Kagame ndiye kiongozi pekee wa Rwanda wengi wamewahi kumfahamu.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66 anasifiwa kwa kujenga upya taifa lililokumbwa na kiwewe baada ya mauaji ya kimbari lakini pia anashutumiwa kutawala katika mazingira ya hofu nyumbani.

Zaidi ya Wanyarwanda milioni tisa - wapatao milioni mbili wapiga kura kwa mara ya kwanza - walijiandikisha kupiga kura zao, huku kinyang'anyiro cha urais kikifanyika kwa wakati mmoja na uchaguzi wa wabunge kwa mara ya kwanza.

'Antupa kila kitu'

"(Kagame) anatupa kila kitu tunachomuuliza, kama vile bima ya afya. Hii ndiyo sababu anashinda kwa kura nyingi," alisema mekanika mwenye umri wa miaka 34 Francois Rwabakina.

Kagame alishinda kwa zaidi ya 93% ya kura mnamo 2003, 2010 na 2017, alipowashinda tena wapinzani hao wawili kwa urahisi.

Katika uchaguzi wa ubunge, wagombea 589 walikuwa wakiwinda viti 80, wakiwemo 53 waliochaguliwa kwa kura ya maoni kwa wote.

Katika bunge lililomaliza muda wake, chama cha RPF cha Kagame kilikuwa na viti 40 na washirika wake 11, huku chama cha Habineza kikiwa na viti viwili. Nafasi nyingine 27 zimetengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

TRT Afrika