Serikali ya Rwanda imepinga kauli ya Mahakama ya Juu ya Uingereza inayoashiria kuwa Rwanda sio salama.
Hii inafuatia uamuzi wa mahakama hio kuwa si ruhusa kwa Uingereza kupeleka wakimbizi nchini Rwanda.
"Huu ni uamuzi wa mahakama ya Uingereza," asema msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo, "Hata hivyo, tunapinga uamuzi kwamba Rwanda si nchi ya tatu salama kwa wanaotafuta hifadhi na wakimbizi katika suala la kuwarudisha nyuma."
Seriklai hiyo imesema inatilia maanani majukumu ya kibinadamu kwa uzito na itaendelea kuyatimiza.
"Rwanda na Uingereza zimekuwa zikifanya kazi pamoja ili kuhakikisha kuwa watu wanaotafuta hifadhi waliohamishwa wanaunganishwa katika jamii ya Rwanda," Makolo ameongezea.
"Rwanda imejitolea kutekeleza majukumu yake ya kimataifa. Tumetambuliwa na UNHCR na taasisi nyengine za kimataifa kwa jinsi tunavyowatendea wakimbizi," Makolo amesema.
Rwanda tayari ina wakimbizi
Rwanda tayari inatoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka nchi kadhaa.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea wakimbizi, UNHCR, zaidi ya wakimbizi 135,000 na wanaotafuta hifadhi wamesajiliwa na UNHCR nchini Rwanda.
Wakimbizi wengi wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi.
Kwa wakimbizi wanaotoka DRC na ambao wameishi Rwanda kwa zaidi ya miaka 25, lengo linabakia katika kujumuishwa kwao katika mifumo ya kitaifa na kuongeza fursa za maisha ili waweze kujitegemea katika maisha.
Tangu Novemba 2022, kutokana na ukosefu wa utulivu unaoendelea Mashariki mwa DRC, idadi ya wanaotorokea Rwanda inaongezeka.
Kwa sasa, takriban wakimbizi 50,000 wa Burundi bado wanaishi Rwanda, huku 21.7% wakiishi mijini, wakati waliosalia wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Mahama.
Rwanda inahifadhi idadi ndogo ya wakimbizi kwa nchi nyingine kama vile Eritrea, Sudan Kusini, Sudan, Somalia na Ethiopia inayowakilisha asilimia 0.03 ya wakimbizi wote.
Rwanda na waliohamishwa Libya
Mnamo Septemba 2019, Rwanda ilitia saini mkataba wa kwanza wa makubaliano (MoU) na UNHCR na Umoja wa Afrika (AU) ili kuwahamisha wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka Libya hadi Rwanda.
Chini ya Makubaliano hayo, UNHCR kwa kushirikiana na Serikali ya Rwanda na AU ilianzisha Mfumo wa Usafiri wa Dharura (ETM) katika Sekta ya Gashora, Wilaya ya Bugesera, Rwanda, ili kusaidia hadi wakimbizi 500 na waomba hifadhi waliohamishwa kutoka Libya.
Mnamo Oktoba 2021, makubaliano haya yaliongezewa muda hadi Desemba 2023.
Kati ya Septemba 2019 na Machi 2023, wakimbizi 1,600 na wanaotafuta hifadhi walihamishwa kutoka Libya hadi nchini Rwanda kupitia safari 13 za ndege za kuwahamisha.
Wakimbizi na wanaotafuta hifadhi wanajumuisha watu kutoka Eritrea, Somalia, Sudan, Ethiopia, South-Sudanese, Cameroon, Nigeria na Chad.
Zaidi ya wakimbizi 900 wamepewa makazi mapya katika nchi za tatu.