Viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Paul Kagame na Félix Tshisekedi wamejadiliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, kuhusu hali ya DRC.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa waziri Blinken alisisitiza suluhisho la kidiplomasia kutuliza mvutano kati ya nchi hizo mbili huku akahimiza kila upande uchukue taratibu za kutuliza hali hiyo, pamoja na kuondoa vikosi vilivyowekwa kwenye mpaka.
Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Matthew Miller, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X, kuwa, Blinken alielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya mashariki mwa DRC na kuunga mkono suluhisho la kidiplomasia.
Kwa upande wake, Ikulu ya Rwanda, imesema kuwa Rais Kagame amehakikisha msaada thabiti wa Rwanda katika mchakato mzima unaoendelea wa kikanda ili kufanikisha amani na utulivu DRC na mkoa huo kwa jumla.
Haya yanajiri baada ya viongozi mbalimbali chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wakiwemo Marais Joao Lourenco (Angola), Felix Tshisekedi (DRC), Samia Suluhu (Tanzania), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Hakainde Hichilema (Zambia) na Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe) kujumuika katika kilele cha mkutano uliofanyika tarehe 04 Novemba 2023, huko Luanda, Angola.
Mkutano huo ulitoa mwongozo wa kimkakati juu ya kupelekwa kwa vikosi vya walinzi wa SADC nchini DRC (SAMIDRC) ili kurejesha amani na usalama nchini humo.
Mkutano huo pia ulieleza wasiwasi wake juu ya kuzorota kwa hali ya usalama na kibinadamu mashariki mwa DRC na taarifa za kuanzika tena kwa mashambulio na uvamizi wa eneo na M23, pamoja na ukiukaji wazi wa kusitisha mapigano.