Waziri wa Uhamiaji wa Uingereza Robert Jenrick alijiuzulu siku ya Jumatano baada ya serikali kuchapisha sheria kuhusu mkataba wake wenye utata na Rwanda wa kutuma wahamiaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Ndani James Cleverly aliwaambia wabunge kwamba Robert Jenrick amejiuzulu, katika hatua ambayo inaleta shinikizo kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak.
Mapema Jumatano Rwanda ilionya kujiondoa katika mkataba wa kuwapokea wahamiaji iwapo Uingereza haitaheshimu sheria za kimataifa.
Uingereza na Rwanda zilitia saini mkataba mpya Jumanne katika jitihada za kufufua pendekezo linaloonekana kuwa na utata la Uingereza la kuwahamisha wahamiaji katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, pendekezo ambalo awali lilipingwa na mahakama ya Uingereza.
Waziri wa Mambo ya Nje Vincent Biruta, ambaye alitia saini mkataba huo wa pande mbili, alisema ukiukaji wowote wa mikataba ya kimataifa unaweza kuifanya Rwanda kujiondoa katika mkataba huo.
'Fanya kihalali'
"Siku zote imekuwa muhimu kwa Rwanda na Uingereza kwamba ushirikiano wetu wa utawala wa sheria unakidhi viwango vya juu zaidi vya sheria za kimataifa, na inaweka wajibu kwa Uingereza na Rwanda kuchukua hatua kihalali," alisema katika taarifa yake.
"Bila y uhalali wa Uingereza, Rwanda isingeweza kuendelea na Ushirikiano wa Uhamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi," aliongeza, akimaanisha mpango huo wenye utata.
Mswada huo unapendekeza kuwapa mawaziri mamlaka ya kupuuza sehemu za Sheria ya Haki za Kibinadamu ya Uingereza na Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu wakati wa kuzingatia kesi za kufukuzwa nchini.
Amri ya mahakama
Sheria ya hapo awali ilikuwa inasema kuwa watu watakaoingia Uingereza kinyume cha sheria watarejeshwa katika nchi yao au kuhamishiwa Rwanda.
Rwanda ingepokea takriban dola milioni 177 ili kupokea wahamiaji wanaoingia Uingereza.
Wahamiaji wa kwanza walipaswa kutumwa Rwanda mwezi Juni mwaka jana lakini waliondolewa kwenye ndege dakika ya mwisho baada ya jaji katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu kutoa amri.
Tangu wakati huo, kesi zao - na uhalali mpana wa sera - zimekwama katika mahakama.
Mwezi Juni mwaka huu mahakama ya rufaa ya Uingereza ilitoa uamuzi kwamba mpango wa serikali ya Uingereza wa kuwapeleka wakimbizi waomba hifadhi nchini Rwanda ni batili kisheria.
Walisema kuwa serikali ya Uingereza haiwezi kuhakikisha kuwa wakimbizi waliotumwa Rwanda hawatarejeshwa katika nchi wanayokimbia.
"Kumpeleka mtu yeyote Rwanda kutakuwa ni uvunjaji wa kifungu cha 3 cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu" ambao unasema kuwa hakuna mtu atakayewekwa katika mateso, matibabu au adhabu ya kikatili au ya kinyama," walisema majaji.
Serikaii ya Rwanda imesisitiza kuwa iko na usalama wa kutosha kwa wahamiaji.
"Rwanda ni mojawapo ya nchi salama zaidi duniani na tumetambuliwa na Shirika la Kutetea Haki za Wakimbizi, UNHCR na taasisi nyingine za kimataifa kwa jinsi tunavyowalinda wakimbizi," msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alisema.
Takriban wahamiaji 30,000 wamevuka kutoka kaskazini mwa Ufaransa kwa meli mwaka huu.