Baada ya kupotosha mamia ya waumini, na baadhi yao kujiua kwa kufunga bila kukula chochote katika juhudi zao za "kumuona Yesu," mhubiri wa kanisa lenye utata la Good News International kutoka Kaunti ya Mombasa nchini Kenya, Paul Mackenzie, amefananishwa na gaidi anayetumia dini kueneza mambo ya ajabu na itikadi zisizokubalika.
“Magaidi hutumia dini kuendeleza vitendo vyao viovu. Watu kama Mackenzie wanatumia dini kufanya jambo lile lile,” alisema Rais William ruto.
Akiongoza sherehe za kufuzu kwa makadeti wa Jeshi la Magereza nchini Kenya Jumatatu, rais Ruto aliwataka Wakenya na mashirika mbalimbali ya serikali kuwa macho dhidi ya wale wanaotaka kupotosha waumini.
“Tunachokiona Kilifi, huko Shakahola, ni sawa na swala la kigaidi.Hakuna tofauti kati ya Mackenzie ambaye anajificha na kujifanya mchungaji ilihali yeye ni mhalifu mbaya,” Ruto alisema.
Paul Mackenzie Nthenge, mhubiri huyo tata, kwa sasa anazuiliwa na polisi akisubiri kufikishwa mahakamani pindi tu uchunguzi utakapokamilika.
Aliwekwa kizuizini mnamo Aprili 15 baada ya miili ya watu wanne kupatikana katika shamba moja ambalo alikua akiendeshea shughuli zake za 'kidini'.
Mhubiri huyo hata hivyo, amenyimwa dhamana licha ya kukana kuhusika na kusisitiza kwamba kanisa lake alilifunga tangu mwaka 2019.
Kulingana na wanafuasi wake, huwa anawaagiza kujinyima chakula hadi “wakutane na Yesu.” .
Kufuatia uchunguzi kuhusu washiriki wa kundi lake, polisi wa Kenya wamefukua mamia ya mabaki ya mili kadhaa kwenye makaburi ya kina kirefu katika eneo la ekari 800 la msitu huko Shakahola, karibu na Malindi eneo la pwani nchini kenya.
Kulingana na habari zilizotolewa na maafisa wa upelelezi, miili 47 imefukuliwa hadi sasa.
"Leo tumefukua miili 26 zaidi na hii inafanya jumla ya miili kutoka eneo hilo kufikia 47," msimamizi wa uchunguzi wa uhalifu huko Malindi, mashariki mwa Kenya, Charles Kamau alisema
Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa wa Kenya Kithure Kindiki pia alitaja ugunduzi huo wa kushtua kama "Mauaji ya Msitu wa Shakahola" katika ujumbe wake wa Twitter siku ya Jumapili, akiahidi hatua kali dhidi ya Mackenzie huku serikali ikijitahidi kuwabana wachungaji walaghai.
‘Nimemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Timu ya Usalama ya Mkoa kuimarisha timu za uchunguzi ifaavyo kabla ya ziara yangu siku ya Jumanne.
Maafisa wa usalama wa kutosha wametumwa na msitu mzima wa ekari 800 umefungwa na kutangazwa kuwa eneo la uhalifu' ulisema ujumbe huo kupitia mtandao wa twitter.
Mackenzie amewahi kuzuiliwa na polisi mara mbili, mwaka 2019 na Machi 2023, kuhusiana na vifo vya watoto wawili.
Aliachiliwa huru kwa dhamana baada ya kusema kutojua hali iliyo zunguka vifo vya watoto hao akidai kwamba amekuwa akizungumziwa vibaya tu mara kwa mara.
Taarifa za mhubiri huyu zimewaacha wengi vinywa wazi huku Miili zaidi ikitarajiwa kufukuliwa na polisi.