Kenya ilifanya mkutano wa dharura kukabiliana na mvua za El Nino ambazo zimeathiri maeneo tofauti ya nchi.
Mkutano huo ulioongozwa na rais William Ruto ulifanywa kufuatia mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya watu, familia kuhama na kuharibu mali.
Baraza la Mawaziri linasema kuwa kaunti 38 ziko katika hatari ya El Nino, idadi ya walioaga dunia imefikia 76 huku 35,000 wakiwa wameyahama makazi yao kufuatia mafuriko yaliyoathiri nchi.
Hata hivyo, serikali inasema haitatangaza hali kuwa janga la taifa.
"Uamuzi wa kutangaza janga la kitaifa unategemea takwimu juu ya ardhi," msemaji wa ikulu Hussein Mohammed amaesema katika mkutano na waandishi wa habari, "data ambayo imetathminiwa inaweka hali ya sasa katika kiwango cha hatua ya kutisha."
Serikali imeamua kuweka hazina ya dharura ya zaidi ya dola milioni arobaini na tano na laki nane ( $45.8M) kukabiliana na El Nino nchini.
Waziri wa afya, Nakhumicha Wafula anasema Mvua kubwa zinazonyesha kwa muda mrefu zinazonyesha kote nchini zina madhara kadhaa katika huduma za afya.
" Athari ya mafuriko ni pamoja na kukatika kwa upatikanaji wa huduma za afya, kupoteza maisha, majeruhi, watu kuhama makazi yao, uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwa ni pamoja na vituo vya afya, na kuzorota kwa kiasi kikubwa kwa maisha ya jamii," amesema.
Serikali imeomba wananchi kutahadhari wanaposafiri na kuripoti visa vyovyote vya mafuriko au maporomoko ya ardhi kwa mamlaka husika.
Hata hivyo rais amekashifiwa kwa kusifu mvua huku yameleta mafuriko katika maeneo tofauti.
" Mvua katika baadhi ya maeneo ya nchi ina manufaa. KCC ( Kampuni ya serikali ya maziwa) imepewa zaidi dola milioni tatu na laki mbili, ili waweze kuchukua maziwa kutoka kwa wakulima, ushuru utapunguzwa kwa watumiaji," Mohammed msemaji wake amemtetea rais.