Mwaka wa 2007 ni mwaka ambao Caroline Njeri hapendi kuukumbuka. Ulikuwa mwaka uliobadilisha maisha yake bila yeye kutarajia.
Baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2007, ghasia za kikabila zilizuka nchini humo.
"Uchaguzi mkuu ulikuwa umekwisha na mara tu tukaanza kusikia fununu kuwa sisi ambao hatukuwa kabila la eneo moja tulilokuwa tukiishi tulitakiwa kuhama," Njeri anaiambia TRT Afrika.
Vita vya kikabila viliwalazimu watu katika maeneo kadhaa nchini Kenya kutafuta zenye usalama kukimbilia.
Vita vilizuka wakati wa makabiliano kati ya wafuasi wa wagombea wawili waliokuwa wanashindana wakati huo, Raila Odinga na Mwai Kibaki, yaliongezeka na kuwa mzozo wa umwagaji damu wa jamii.
Njeri alikuwa mzaliwa wa Kericho eneo ambalo ni makao ya kabila la Kalenjin. Kwa sababu alikuwa natoka kabila la Wakikuyu, uwepo wake katika eneo hilo ulihatarisha maisha yake. Vile vile watu wa asili ya Kalenjin ambao walikuwa wakiishi katika maeneo mengine ambayo yalikuwa ya Wakikuyu nao pia walijikuta wanalazimika kuhama.
"Mimi na mwanangu wa miaka saba tulilazimika kulala katika uwanja wa serikali ambapo watu wengi walikuwa wamekimbilia kama eneo salama pekee, kwa sababu angalau kulikuwa na ulinzi wa jeshi," Njeri anasema huku akiwa katika dimbwi la mawazo.
"Hapo sasa tulikuwa hatujui vipi au lini tutapata usafiri wa kuondoka mji wa Kericho, lakini cha kusikitisha zaidi ni kuwa hatukuwa tunajua tutaenda wapi, ilhali maisha yetu yote yalikuwa katika mji wa Kericho, ilikuwa wakati mgumu sana maishani hasa kwa watu kama sisi wenye watoto."
Nae Bwana James Keroga mwenye umri wa miaka 78 sasa anasema hataku kukumbuka yaliyojiri mwaka 2007 na 2008.
" Niliwacha biashara yangu ya miaka 40, sikuwa na uwezo na muda wa kuiokoa, nilionywa na marafiki zangu kuwa kuna watu ambao wangenishambulia siku ya Jumatatu, hivyo niliinuka hata bila begi na kuelekea katika mji jirani wa Nakuru," Karoga anaiambia TRT.
"Ilibidi magari tuliyopanda yasindikizwe na wanajeshi kutoka mji mmoja hadi mwingine kwa sababau, hata barabarani kulikuwa na makundi yenye silaha ambayo yalikuwa yanashambulia watu kwa misingi ya kikabila," Keroga anaongezea.
Wakati mgumu Kenya
"Huo ulikuwa wakati mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya taifa letu, wakati ambapo mwananchi wa kawaida hakuwa na uwezo wowote wa kujisaidia kwa sababu ilikuwa mwananchi mmoja dhidi ya mwengine, majirani walikuwa maadui, jamii yetu ilishuhudia wakati wa giza sana."
Zaidi ya watu 1,000 waliauwa kutokana na ghasia hizo na wengine 600,000 kukimbia makazi yao. Waliokuwa na jamaa na marafiki wa kuwasaidia walifaidika kiasi lakini wengine walikimbilia katika makambi ambazo zilikuwa zimewekwa katika maeneo tofauti nchini.
Mnamo tarehe 31 Machi 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, ilifungua kesi kuhusiana na madai ya uhalifu wa kibinadamu uliofanywa kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka wa 2007 na 2008.
Uchunguzi wa ICC ulizingatia madai ya uhalifu dhidi ya binadamu katika maeneo sita kati ya nane nchini Kenya, ambayo ni Nairobi, Bonde la Ufa Kaskazini, Bonde la Ufa la Kati, Bonde la Ufa Kusini, Mkoa wa Nyanza na Mkoa wa Magharibi.
Kutafuta haki kwa mahakama ya ICC
Mwendesha mashtaka wa ICC alitaja washukiwa sita:
Meja Jenerali Mohammed Hussein Ali – wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi alikuwa Kamishna wa Polisi wa Kenya.
Uhuru Muigai Kenyatta - aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu wa wakati huo na Waziri wa Fedha, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa chama cha kisiasa cha KANU, ambacho kiliunga mkono Chama cha Rais Mwai Kibaki cha Umoja wa Kitaifa wakati wa uchaguzi uliohusika.
Henry Kiprono Kosgey - aliyekuwa Waziri wa Viwanda wakati huo na mbunge wa jimbo la Tinderet, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Orange Democratic Movement.
Francis Kirimi Muthaura - aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma wakati huo, Katibu wa Baraza la Mawaziri na mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Usalama.
William Samoei Ruto - aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia wakati huo na mwanachama wa ODM katika Bunge la Kitaifa la Eneo Bunge la Eldoret Kaskazini.
Joshua Arap Sang - aliyekuwa mkuu wa operesheni katika kituo cha redio cha lugha ya Kalenjin KASS FM, ambaye wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi alikuwa mtangazaji wa redio.
Afueni ama hakuna tofauti?
" Mashtaka yote dhidi ya washukiwa hawa sita hayakuthibitishwa au yaliondolewa au kusitishwa bila upendeleo," mahakama ya ICC imesema katika taarifa.
Hata hivyo, uchunguzi uliendelea na washukiwa wengine watatu wakatajwa, mmoja alifariki na wawili bado hawajawahi kufikishwa mbele ya mahakama hii.
Mahakama ya ICC sasa imefunga kesi ya Kenya.
"Baada ya kutathmini taarifa zote nilizonazo kwa wakati huu, nimeamua kuhitimisha awamu ya uchunguzi katika hali nchini Kenya," naibu mwendesha mashtaka wa ICC, Nazhat Shameem Khan alisema katika taarifa yake. "Ofisi haitafuatilia kesi za ziada katika madai ya jinai ya watu wengine."
Waathirika wa moja kwa moja wa vurugu za mwaka 2008/2009 wana hisia tofauti.
" Hatujapata haki, sisi ambao tulidhumumiwa," Njeri anaiambia TRT Afrika, "kwa sababu hakuna ambaye alitusaidia kurejesha maisha yetu katika hali ambayo ilikuwa hapo awali, tumeng'a nga'na peke yetu."
"Taarifa hii ya ICC kufunga kesi ya Kenya haitusaidii chochote, hata hainijalishi mimi, hata kama wangefungwa, bado maisha yangu yangebaki pale pale, ya kujisaidia kujimudu kisaikolojia na kimaisha."
"Hao ni watu tisa tu ambao walipelekwa mahakamani, na je wale maelfu ambao walitufukuza moja kwa moja je? Nani atawaadhibu hao? Uamuzi huo hautuhusu sisi kabisa," Mzee Keroga anauliza.