Rais wa Kenya Wiliam Ruto amesema yupo tayari kufanya maongezi na viongozi wa mahakama na wa kibunge ili kutatua mvutano ambao umejitokeza hivi majuzi.
Vita vya maneno vimezuka kati yake na mahakama huku akionekana kuutisha mhimili wa mahakama, kwa madai kuwa, baadhi ya majaji wamepokea rushwa kwa ajili ya kuangusha miradi yake ya maendeleo.
Jaji mkuu wa Kenya Martha Koome aliitisha majadiliano na rais kuongea kuhusu mzozo kati ya vitengo hivyo vya serikali.
"Mimi nataka nimwambie jaji mkuu, mimi niko tayari," rais Ruto amesema Jumanne.
Rais Ruto alidai kuwa baadhi ya maamuzi yaliyotolewa na Idara ya Mahakama yanapunguza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya serikali yake.
Mahakama Kuu mwaka jana ilisitisha ushuru wa nyumba wenye utata na ushuru wa hazina ya afya na pia imesitisha uuzaji uliopangwa wa mashirika kadhaa ya serikali. Maamuzi ya mwisho yanatarajiwa mwaka huu.
"...Kuna maafisa wengi wazuri katika mahakama na tutang'oa wafisadi. Tutafanya hilo,,," rais Ruto alisema mapema mwezi huu katika ujumbe wake katika mtandao wa X.
Idara ya mahakama nchini humo ilimkosoa rais Ruto kutokana na matamshi yake kuwa kuna baadhi ya majaji "wafisadi" waliokuwa wakipanga njama na "makampuni" ili kukatisha tamaa serikali kupitia mfumo wa mahakama.
Jaji Mkuu Martha Koome alionya juu ya hatari ya "machafuko" ikiwa uhuru wa mahakama hautaheshimiwa.
"Wakati maafisa wa serikali au wa umma wanatishia kukaidi maagizo ya mahakama, utawala wa sheria unahatarishwa, na kuweka mazingira ya machafuko kutawala katika taifa," Koome alinukuliwa akisema katika risala ya ndani, bila kumtaja Ruto moja kwa moja.
Wilki iliyopita mawakili chini ya muungano wao wa Law Society of Kenya walifanya maandamano wakipinga kile amabcho walidai, uingiliaji wa mahakama na vitisho kutoka kwa rais Ruto.
Rais huyo ambaye aliingia mamlakani mwaka 2022 baada ya mahakama kuamua kuwa uchaguzi wa Agosti 2022 ulimpa ushindi halali, sasa anaonekana kutafuta suluhu kwa mvutano wake na mahakama.
"Niko tayari kwa majadiliano ya jinsi tutakavyoshughulikia masilahi, kama uzembe na haswa ufisadi iwe kwenye bunge, mahakama au serikalini, kwa sababu inachelewesha na inaharibu maendeleo ya Kenya," rais amesema.