Rais Yoweri Museveni amesifia lugha ya kiswahili kama njia ya mawasiliano ambayo haina mvutano.
"Tuna lahaja isiyopingwa. Hii ni Kiswahili," Rais Museveni alisema akiwa Ikulu ya Nairobi katika ziara yake rasmi Kenya.
"Sisi sio kama Umoja wa Ulaya ambao hawana lugha. Wanapokutana Brussels hawawezi kuzungumza. Mtu anazungumza Kijerumani, mwingine anazungumza lugha nyengine … kupitia earphone… unapomaliza unakaribia kuwa kiziwi," Museveni alisema.
Hotuba ya rais Museveni imelenga umuhimu wa Afrika kutafuta misingi ya amani na umoja katika bara la Afrika, akihimiza kuwa nchi za Afrika Mashariki tayari zinaunganishwa na utamaduni tofauti.
"Unaweza kuwa na nchi ndogo duniani…kama Denmark, Ubelgiji lakini wana “kinara” ambaye anayewahakikishia, hii ni Marekani. Wanapokuwa hatarini “kinara” anakuja kuuliza “ni nini kinatokea hapa?” Sasa "kinara" wa Afrika ni nani? "Sisi sote ni watu wadogo wadogo hapa na pale na hii ndio tunajaribu kufanyia kazi," Rais Museveni alisema.
Kenya na Uganda zimetia saini makubaliano saba ya ushirikiano.
Hizi ni pamoja na ushirikiano katika mafunzo ya kidiplomasi, ushirikiano wa huduma za umma na masuala ya vijana ya pamoja, katika michezo na katika amani na usalama.
"Tumekubaliana pia kuhakikisha kuwa biashara kati ya nchi zetu mbili haziathiriwi na vikwazo vyovyote, kwa hivyo masuala yote yaliyopinga biashara yetu ya mchele, kuku, sukari, vyombo vya mbao zimetatauliwa," Rais William Ruto alisema.
"Pia tumekubaliana kwa pamoja tutahakikisha tunajenga mabomba ya mafuta kutoka Eldoret hadi Kampala," rais Ruto aliongezea.
"Tulieleza wasiwasi kuhusu kuondoka kwa ATMIS nchini Somalia na tulihimiza kwamba kalenda za wakati wao kuondoka Somalia iambatane na usalama nchini humo na sio tu tarehe ya kalenda iliyopangwa," Rais Ruto ameongezea.
ATMIS ni wanajeshi wa Afrika walio nchini Somalia kwa ajili ya kusaidia nchi hiyo kulinda amani dhidi ya changamoto kama wanamgambo wa Al Shabaab.
Kwa makubaliano ya Umoja wa Afrika na Somalia wanajeshi wa kikosi hiki wanafaa kuanza kuondoka nchini humo na kuacha jukumu la usalama kwa jeshi la Somalia kufikia mwisho wa 2024. Kufikia Februari mwaka huu wanajeshi 5000 walikuwa wameondoka ikiwa askari 4000 wanatarajiwa kupunguzwa kufikia mwezi Juni mwaka huu.
ATMIS ambayo hapo awali iliitwa AMISOM, ilikuwa na zaidi ya wanajeshi 18,000 ikiwa wanajeshi waliingia Somalia 2007 kusaidia nchi hiyo kuimarisha usalama.