Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. 

Haya yanajiri siku chache tu baada ya serikali ya Uingereza kutoa tahadhari ya uwepo wa ongezeko la tishio la ugaidi nchini Uganda, yaliyowalenga raia wa kigeni.

Museveni ameyasema hayo akirudi kutoka Abu Dhabi, ambapo alikwenda kukutana na rais wa UAE, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan.

Serikali tatu za Magharibi zikiwemo Marekani, Uingereza na Ireland ziliwaonya raia wao kujiepusha na tamasha kubwa la muziki lililokuwa likifanyika jinja, Uganda.

"Nimesikia kuwa Wamarekani na Waingereza wenye woga walituma kile wanachokiita ushauri kwa raia wao wasije Uganda. Ushauri huu wa baadhi ya watendaji hawa ni aina nyingine ya kuingilia mambo yetu ya ndani," Museveni amesema.

Aidha, Marekani ilitoa taarifa ikiwashauri raia wake kutohudhuria tamasha hilo, kwa sababu za kiusalama."

Museveni ametofautiana nao huku akisema tahadhari hizo hazikustahili.

"Iwapo hali ingekuwa mbaya sana, ni sisi ndio tungewashauri watu wasije Uganda, sio Waingereza na Wamarekani," aliandika kwenye mtandao wa X.

Museveni ameyalaumu mataifa hayo kwa kuchagia kwa kuzorota kwa usalama barani.

"Baadhi ya ugaidi Afrika unafanywa na baadhi ya wahusika wanaojidai polisi wa kimataifa. Machafuko ya Libya na nchi zinazozunguka Sahel (Mali, Burkina-Faso, Niger, Nigeria, Chad,) yanatokana na baadhi ya wahusika hao."

Tahadhari hizo zilitolewa baada ya Uganda kushuhudia mashambulio kadhaa yaliyolaumiwa kwa wanamgambo wanaoshirikiana na kundi la Daesh lenye makao yake katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

"Kwa bahati nzuri, Uganda ya Leo ina uwezo wa kutoa mchango muhimu katika, angalau, sehemu za Afrika jirani nasi. Tutashinda," Museveni alimaliza.

Mwezi uliopita, watalii wawili wa kigeni waliokuwa fungate na mwenyeji wao wa Uganda waliuawa katika mbuga ya kitaifa katika shambulio ambalo lilidaiwa na kundi la Daesh.

TRT Afrika