Na Kevin Philips Momanyi
Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga atalazimika kusubiri hatma ya mapendekezo na mabadiliko katika utaratibu wa kumchagua mrithi wa Moussa anayemaliza muda wake kama mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, baadae mwaka huu.
Mabadiliko hayo yanaziondolea sifa nchi wanachama wa AU zilizowahi kushika nafasi za uenyekiti na makamu mwenyekiti, kati ya mwaka 2002 mpaka leo.
Chaguzi hizo zitafanyika kwenye mkutano wa AU, mwaka 2025.
Mbali na Kenya, nchi nyingine inayosubiria maamuzi ya wakuu wa AU ni Rwanda, ambayo ilitoa makamu mwenyekiti kwenye umoja huo.
Ndoto za Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya zitayeyuka iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa na wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika.
Erastus Mwencha, kutoka Kenya, alihudumu katika Umoja wa Afrika, kama makamu mwenyekiti, kati ya mwaka 2008 hadi 2017.
Tume ya Umoja wa Afrika imekuwa na utaratibu wa kupokezana nafasi ya uenyekiti kwa mzunguko kulingana na maamuzi yake ya mwaka 2018, na kwa sasa, zamu ilidondokea katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hatua hii inakuja wakati Odinga ameungwa mkono na Rais wa Kenya, William Ruto na Yoweri Museveni kutoka Uganda na kiongozi wa zamani na mwanasiasa mkongwe barani Afrika, Olusegun Obasanjo wa Nigeria.