Mwanasiasa mkongwe nchini Kenya, Raila Amolo Odinga./Picha: Getty

Kwa kauli yake mwenyewe aliyoitia Oktoba 13, Raila ambaye anagombea nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) amesema kuwa Adani ni kampuni yenye uzoefu mkubwa kwenye masuala ya kibiashara akisisitiza kuwa hakuna haja ya kutilia shaka utendaji kazi wa kampuni hiyo.

Raila amedai kuifahamu kampuni ya Adani Holdings Limited wakati akiwa Waziri Mkuu wa Kenya.

"Niliifahamu kampuni hii nikiwa kama Waziri Mkuu wa Kenya mara baada ya kuitembelea India mwaka 2010, kampuni hii haina kashfa yoyote kama inavyodaiwa na baadhi ya watu," alisisitiza Raila.

Kwa mujibu wa Raila, kampuni ya Adani Holdings Limited ina thamani ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 200, na hivyo ni ajabu kwa watu kuanza kuihusisha kampuni hiyo na vitu visivyoeleweka.

Baadhi ya wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya wakiandamana siku ya Septemba 11 kupinga hatua ya kuipa kampuni tenda ya kuendesha uwanja huo./Picha: Getty

"Ni vyema kuondoa sintofahamu zozote kuhusu kampuni ya Adani kwani ni taasisi yenye uzoefu mkubwa katika biashara za namna hiyo," alisema.

Kulingana na Raila, mpango wa kuipa kampuni ya Adani tenda hizo ni wa uhakika kwani kwa sasa, Kenya haina fedha za kutosha za kupanua uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na kushughulikia huduma za nishati ya umeme.

Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya, alitaka uwazi utawale kwenye utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza haja ya kuheshimu matakwa ya Wakenya.

Kauli ya Raila inakuja huku kukiwa na kesi mahakamani ya kupinga uamuzi wa kuipa kampuni hiyo tenda ya kuendesha uwanja wa JKIA.

Uamuzi kuhusu uendeshaji wa uwanja wa JKIA utatolewa siku ya Oktoba 25, 2024.

Tayari, kampuni hiyo imetenga kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 1.3 kwa shughuli ya kusambaza umeme na zingine bilioni 1.85 kwa ajili ya upanuzi wa JKIA.

TRT Afrika