Sehemu ya muonekano wa ndani wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA)./Picha: Getty

Ukanda wa Afrika Mashariki unashuhudia kasi ya uwekezaji wa makampuni kutoka nje, katika baadhi ya miundombinu yake.

Kati ya miundombinu ambayo inatolewa macho na wawekezaji wa kigeni, ni katika sekta ya usafirishaji.

Hivi karibuni, kampuni hiyo kutoka India ya Adani Group, kupitia kampuni yake tanzu ya Adani Airport Holdings Limited, ilionesha nia ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Tayari, wawekezaji hao wametenga kiasi cha dola bilioni 1.85 kupanua sehemu ya uwanja wa ndege wa Kimaitaifa wa Jomo Kenyatta.

Iwapo mchakato huo utaidhinishwa, basi kampuni hiyo kutoka India itakuwa imejihakikishia kukusanya asilimia 18 ya mapato yake ya kila mwaka, ndani ya miaka 30, tangu kuanza kwa uwekezaji huo.

Kampuni hiyo pia imelenga kubadilisha muonekano wa JKIA, ikiwa ni pamoja na kujenga sehemu ya pili ya kurukia ndege ndani ya uwanja huo wa kimataifa nchini Kenya.

Mchanganuo zaidi unaonesha kuwa kampuni ya Adani itatumia dola milioni 750 kujenga jengo la abiria, sehemu ya maegesho ya ndege na sehemu za kutokea.

Mradi huo, unategemewa kukamilika ifikapo mwaka 2029.

Mbali na Kenya, kampuni ya Adani Group, pia imewekeza nchini Tanzania.

Kupitia mpango wa APSEZ, kampuni ya Adani ilishinda zabuni ya kuendesha yadi ya makontena katika bandari ya Dar es Salaam, kwa miaka 30.

Muonekano wa Bandari ya Dar es Salaam, nchini Tanzania./Picha: Reuters

Mpango huo ni muendelezo wa ushirikiano kati ya Adani na bandari za Abu Dhabi, ulioasisiwa mwaka 2022, ukijulikana kama 'East Africa Gateway'.

“Dar es Salaam ni sehemu ya kimkakati ikiwa imeunganishwa vizuri miundombinu ya reli na barabara,” imesema APSEZ.

“Nina imani yangu kuwa uzoefu wetu katika bandari na usafirishaji, utatuwezesha kuongeza ujazo wa kibiashara na uhusiano wa kiuchumi kwenye bandari zetu za Afrika Mashariki,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa APSEZ Karan Adani.

Kiu ya kuwekeza kwenye bandari nchini Tanzania, kunatokana na ukaribu wa nchi hiyo na nchi zingine zisizokuwa na bahari kama vileMalawi, Zambia, DRC, Burundi, Rwanda na Uganda.

TRT Afrika