Paul Kagame ala kiapo cha kuiongoza Rwanda kwa awamu ya nne

Paul Kagame ala kiapo cha kuiongoza Rwanda kwa awamu ya nne

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekula kiapo cha kuiongoza nchi hiyo kwa mara ya nne.
Paul Kagame alipata asilimia 99 ya kura zote katika uchaguzi wa nchi hiyo uliofanyika Julai 15, 2024./Picha: AA

Siku ya Jumapili, Rais wa Rwanda alikula kiapo cha kuiongoza nchi hiyo baada ya ushindi wake wa kishindo ambapo alipata asilimia 99 ya kura zote katika uchaguzi uliofanyika Julai 15.

Viongozi mbalimbali kutoka nchi tofauti barani Afrika walihudhuria hafla ya kumuapisha kiongozi huyo katika jiji la Kigali.

Akiapishwa na Jaji Mkuu Faustin Ntezilyayo, Kagame aliahidi "kudumisha amani, umoja na mshikamano wa nchi hiyo."

Akabiliana na wagombea wawili

Alipata asilimia 99.18 ya kura zote zilizopigwa na hivyo kujihakikishia miaka mingine mitano madarakani, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi.

Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo wanasema kuwa ushindi wa kishindo wa kiongozi huyo mwenye miaka 66, ni uthibitisho tosha wa kukosekana kwa demokrasia nchini Rwanda.

Kiongozi wa chama cha Democratic Green Party Frank Habineza alijinyakulia nafasi ya pili kwa asilimia 0.5 ya kura dhidi ya 0.32 za Philippe Mpayimana, ambaye alishiriki kama mgombea huru.

Mazungumzo ya kumaliza vita na DRC

Kagame anasifiwa kwa kujenga upya taifa lililoharibiwa vibaya na mauaji ya halaiki, ambapo Wahutu wenye itikadi kali walipowauwa Watutsi wachache, na kuua takriban watu 800,000, hasa Watutsi lakini pia Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Lakini wanaharakati wa haki za kibinadamu na wapinzani wanasema anatawala katika hali ya hofu.

Kigali pia inashutumiwa kwa kuchochea ukosefu wa utulivu mashariki mwa jirani yake kubwa zaidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais wa Angola Joao Lourenco, ni kati ya viongozi waliohudhuria shughuli hiyo na alikuwa anategemewa kuwa na mazungumzo ya faragha na Kagame kuhusu usitishwaji wa vita.

Mashambulizi ya M23

Luanda iliafiki makubaliano hayo mwezi uliopita baada ya mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa DRC na Rwanda, ambayo inatuhumiwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 linalopambana na jeshi la Kinshasa.

Hata hivyo, mnamo Agosti 4, siku ambayo mpango huo ulipaswa kutekelezwa, waasi wa M23 - ambao wameteka eneo la mashariki tangu kuanzisha mashambulizi mapya mwishoni mwa 2021 - waliteka mji ulio kwenye mpaka na Uganda.

Katika taifa ambalo asilimia 65 ya watu wake wana umri wa chini ya miaka 30, ni Kagame pekee anayejulikana kama Rais wa nchi huyo.

"Nimejivunia kumpigia kura Rais Kagame na kuipa kipaumbele siku hii," Tania Iriza, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 27, anasema.

'Mabadiliko'

"Uongozi wake umekuwa wa kuleta mageuzi kwa taifa letu. Chini ya uongozi wake, Rwanda imeibuka kutoka katika siku zetu mbaya na kutengeneza njia kuelekea ustawi, umoja na uvumbuzi."

Kagame ameshinda kila uchaguzi wa urais alioshiriki, kila mara kwa zaidi ya asilimia 93 ya kura.

Mnamo 2015, alisimamia marekebisho ya katiba yenye utata ambayo yalifupisha mihula ya urais hadi miaka mitano kutoka saba lakini akabadilisha muhula wa Urais hadi 2034.

TRT Afrika