Nchi ya Rwanda inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Julai 15, 2024, uchaguzi wake wa nne toka machafuko ya mwaka 1994, yalioua Watutsi na Wahutu 800,000 mwaka 1994.
Paul Kagame
Rais Paul Kagame, ambaye amekuwepo madarakani kwa miaka 20 sasa, anawania nafasi nyingine katika uongozi wa juu wa nchi hiyo kupitia chama tawala cha Rwanda Patriotic Front (RPF).
Rais Kagame alishinda uchaguzi wa mwaka 2017 kwa karibu asilima 99 ya kura zote zilizopigwa.
Kagame, ambaye ni kiongozi wa zamani wa waasi, alipata urais Aprili 2000 lakini amekuwa akionekana kama kiongozi wa nchi hiyo tangu mwisho wa mauaji ya kimbari ya 1994.
Mnamo 2022 alipoulizwa kama angejaribu kusaka kuchaguliwa tena, Kagame alisema "atafikiria kuwania kwa miaka mingine 20".
Kiongozi huyo amekabiliwa na ukosoaji kutoka makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kukandamiza upinzani - lakini ametetea vikali rekodi ya Rwanda kuhusu haki za binadamu, akisema nchi yake inaheshimu uhuru wa kisiasa.
Frank Habineza
Akiwa ndiye mwanzilishi wa chama kipekee cha siasa kilichochaguliwa nchini Rwanda, Frank Habineza amewahi kuhudumu kama Naibu Waziri katika Serikali ya Rwanda, na pia amewahi kufanyia kazi vyombo mbalimbali vikiwemo Rwanda Newsline na Rwanda Herald.
Mwaka 2010, Habineza alilazimika kutafuta hifadhi ya kisiasa nchini Sweden ambako aliishi mpaka mwaka 2012. Alifanikiwa kukisajili chama cha DPGR mnamo mwaka 2013, na alitunukiwa shahada ya udaktari wa heshima kutoka chuo kikuu cha Bethel nchini Marekani mwaka 2013.
Juni 7 mwaka huu, tume ya taifa ya Uchaguzi ya Rwanda ilipitisha jina lake kama mgombea wa kiti cha Urais na hivyo kuwa na siku chache za kufanya kampeni.
Ameahidi kupambana na tatizo la ajira na licha ya kwamba hakuwa wazi kumkosoa Rais Kagame, Habineza hajasita kukosoa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na serikali dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
“Tuna nia ya kurejesha demokrasia nchini Rwanda. Demokrasia haitotoka mbinguni, Marekani au hata Ulaya, sisi pekee ndio tunaopaswa kuipigania,” ameongeza Habineza.
Philippe Mpayimana
Kwa sasa, Mpayimana ni mtaalamu mwandamizi kutoka taasisi MINUBUMWE, nafasi aliyoshikilia kutoka Novemba 2021.
Hii ni mara ya pili kwake kugombea nafasi hiyo ya juu nchini Rwanda baada ya kujaribu hivyo mwaka 2017 na kuambulia asilimia 0.72 ya kura zote kwenye uchaguzi ambao Rais Paul Kagame alishinda kwa kishindo.
Kabla ya kujiunga na MINUBUMWE, Mpayimana aliwahi kufanya kazi kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya Rwanda kuanzia mwaka 1990.
Mpayimana na shahada ya uzamili katika lugha, historia na jiografia kutoka chuo kikuu cha Cergy Pontoise nchini Ufaransa na shahada ya uzamili katika uandishi wa habari kutoka chuo kikuu cha Ecole Supérieure de Journalisme cha nchini Ufaransa.
Mbali na siasa, Mpayimana ni mwanaharakati wa haki za binadamu, na pia amekuwa akifundisha masomo ya Kifaransa, Historia na Jiografia katika shule mbalimbali nchini Rwanda, toka mwaka 2013.