Jumuiya ya EAC yajimizwa kuondoa vikwazo vya biashara baada ya kushuka kwa kiwango cha biashara hadi 15%. /Picha: EAC

Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Sekta za Miundombinu, Uzalishaji, Jamii na Siasa, Andrea Aguer Ariik Malueth, alisema lengo kuu la kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu kwenye Ukanda wa Kaskazini na Kati ni kurahisisha usafiri wa watu na kuimarisha usafiri, biashara ya kikanda ambayo bado iko chini na kwa sasa imefikia 15%.

"Biashara ya ndani ya kikanda huko Uropa, Asia na Amerika Kusini ni takriban 60%. Biashara ya ndani ya kanda inaweza kukuza ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ndani ya jumuiya ya kiuchumi ya kanda, pamoja na kuongeza mtiririko wa biashara na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje,” alisema Ariik.

Ameyasema hayo mjini Mombasa nchini Kenya alipokuwa akiongoza Kikao cha 19 cha Mawaziri wa Baraza la EAC kujadili Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa.

Aidha, Ariik alifichua kuwa katika usafiri wa reli, nchi washirika zinaendelea na miradi ya kufanikisha Mtandao wa Reli wa Afrika Mashariki unaounganishwa kupitia Reli ya Standard Gauge na kuipongeza Tanzania kwa uzinduzi wa hivi karibuni wa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Vile vile Ariik alisema, “Jumla ya Km 1,120 za treni ya SGR zinafanya usafiri kazi nchini Kenya na Tanzania, kilomita 1,100 zaidi zinaendelea kujengwa nchini Tanzania na takriban kilomita 4000 ziko katika maandalizi ya mradi katika mataifa yote washirika. EAC itafanya kazi kuhakikisha utendakazi katika mtandao wa kikanda.”

Alisisitiza ya kwamwa ili kufikia muunganisho wa mfumo wa reli, ni lazima kuwe na ushirikiano katika uhamasishaji wa pamoja wa rasilimali ili kuhakikisha hakuna mapungufu ambayo yatasababisha mpango huo kutofanya kazi.

Naye Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa Kenya, Davis Chirchir, mnamo Oktoba 25 alisisitiza umuhimu wa usafiri katika kuimarisha usafiri wa watu, bidhaa, huduma, na rasilimali na kuboresha masoko ya ndani na ya kimataifa.

Chirchir pia alitaja umuhimu wa mfumo wa digitali katika kukuza muunganisho na ukuaji wa uchumi, akibainisha kuwa katika enzi ya kisasa ya kidijitali, mawasiliano ndio daraja linalounganisha mataifa na taasisi zote, kuvuka mipaka ya kijiografia.

"Ni kupitia mifumo madhubuti ya mawasiliano ambapo tunaweza kubadilishana maarifa, kukuza uvumbuzi na kujenga jumuiya yenye mshikamano," alisema.

Chirchir alisema kuwa hali ya hewa ina nafasi muhimu katika kuwezesha ukanda huo kutabiri na kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya asili.

"Takwimu sahihi za hali ya hewa kwa wakati unaofaa ni muhimu kwa kupanga na kulinda miundombinu yetu, kilimo na jamii," alisema.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Dieuconne Dukundane, Waziri wa Miundombinu, Vifaa na Makazi ya Jamii wa Burundi; Jimmy Gasore, Waziri wa Miundombinu wa Rwanda; Dennis Londo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, na Godfrey Baluku, Waziri wa Nchi wa Uganda ICT na Mwongozo wa Kitaifa.

TRT Afrika