Mwanasiasa wa Kenya Raila Odinga asherehekea miaka 80 ./Picha:AFP 

Mmoja wa viongozi wakongwe wa siasa nchini Kenya na anayefahamika kama mwanamageuzi Raila Odinga ametimiza miaka 80 tarehe 7 Januari mwaka huu.

Amekuwa nguzo muhimu katika siasa za nchi hiyo. Ana ushawishi mkubwa kwa wanaomuunga mkono na amekuwa na mchango mkubwa takriban katika kila serikali, licha ya yeye mara nyingi kuwa upande wa upinzani.

Raila Odinga na Rais William Ruto 

Tupate kumfahamu zaidi Raila Odinga

Raila Amolo Odinga alizaliwa Januari 7 mwaka 1945. Amekulia katika mazingira ya siasa ambapo baba yake Mzee Jaramogi Oginga Odinga alikuwa mmoja wa wapigania uhuru wa Kenya na kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa taifa hilo.

Alikuwa kwenye nafasi hiyo kwa kipindi cha chini ya miaka miwili. Raila Odinga pamoja na baba yake walikuwa miongoni mwa wanasiasa waliopigania kuwepo kwa siasa za vyama vingi katika miaka ya themanini na tisini

Raila aliwahi kufungwa gerezani kwa kuhamasisha kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa.Amegombea urais mwaka 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022, kwa ujumla mara tano, ila hajapata fursa ya kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki, lakini amekuwa na mchango muhimu kwa kila serikali iliyokuwa madarakani.

Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2002, chama cha Raila kilijiunga na serikali ya rais wa awamu ya pili Daniel Arap Moi na akawa Waziri wa Nishati.

Mwaka 2002 akasaidia upinzani ulioongozwa na rais wa awamu ya tatu Mwai Kibaki kupata ushindi mkubwa dhidi ya Uhuru Kenyatta na chama cha KANU.

Kugombea Urais

Mwaka 2007 aligombea Urais dhidi ya Mwai Kibaki, ambapo Kibaki alitangazwa mshindi katika uchaguzi uliokuwa na utata. Kutokana na vurugu zilizoikumba Kenya na juhudi za upatanishi, Raila Odinga akateuliwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya maridhiano.

Mwaka 2013 na 2017 aligombea Urais dhidi ya Uhuru Kenyatta. Mwaka 2018 Raila na Uhuru wakafanya makubaliano ya kihistoria maarufu ‘’handshake’’ kuahidi kufanya kazi pamoja na baada ya hapo Uhuru kumuunga mkono Raila katika kuwania Urais.

Mwaka 2022 akashindwa kwenye uchaguzi wa Urais na aliyekuwa makamu wa Uhuru Kenyatta, William Ruto. Na kama inavyosemekana katika siasa yeye ni kama maji ukimkosa kwenye chakula utampata kwenye mchuzi.

Wagombea wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika picha na  Raila Odinga

Licha ya kuwa nje ya serikali, mchango wake bado ulionekana baada ya vurugu za vijana maarufu Gen Z, mwaka 2024, ambapo alionekana kufanya tena ‘’handshake’’ na serikali ya Ruto, hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa upinzani kujumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Mwezi Februari mwaka 2025 Raila Odinga atakuwa anawania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Raila atakabiliana na Mahamoud Ali Youssouf Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti mwenye umri wa miaka 59 na Richard Randriamandrato, aliyekuwa Waziri wa Mambo Nje wa Madagascar mwenye umri wa miaka 55

Baadhi wanahoji, kutokana na umri wake je ataweza mikiki mikiki ya nafasi hiyo?

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika