Baadhi ya viongozi wa Kenya wamelalamikia matamshi ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda akimshutumu mmoja wa wabunge wa Kenya kwa kuchochea upinzani ndani ya nchi yake.
Rais Museveni alimshutumu mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kwa kujihusisha na upinzani na hata kuchangia na kuchochea vurugu.
Katika hotuba yake alipohudhuria hafla ya kumuidhinisha Raila Odinga kugombea Uenyekiti wa Tume ya AU jijini Nairobi, Museveni alisema kuwa anazo taarifa za kijasusi zinazomhusisha Mbunge Owino na upinzani nchini Uganda.
''Mimi napokea rupoti za kijasusi, na baadhi ya watu katika kundi la Raila Odinga hawajui wanachofanya. Kuna mhusika anayeitwa Babu Owino ambaye anajihusisha na chuki dhidi ya NRM ili kuchochea fujo nchini Uganda,'' alisema Museveni.
Hata hivyo matamshi yake yamezua ghadhabu miongoni mwa baadhi ya viongozi wa Kenya wanaodai kuwa yanakiuka itifaki za kidiplomasia na kudhalilisha uhuru wa nchi.
''Chochote ambacho Museveni anacho na Babu Owino, napinga vikali namna alivyomshambulia kiongozi kijana wa Kenya katika ardhi yetu,'' alisema Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. ''Kenya ni nchi inayotawaliwa na sheria na ikiwa kuna tabia yoyote isiyofaa kwa upande wa Babu, kuna njia za kidiplomasia kufikisha hilo kwa Mamlaka za Kenya na kuruhusu sheria kuchukua sababu yake. Lakini kutumia Jukwaa la Urais kutoa shutuma hizo nzito dhidi ya Mkenya ni HAPANA!'' aliongeza Seneta Sifuna.
Naye Babu Owino amemjibu kiongozi huyo wa muda mrefu wa nchi jirani ya Kenya kwa kusisitiza anayo haki y akupigania demokrasia kama kiongozi Afrika.
“Namshukuru Rais Museveni kwa kuunga mkono azma ya Baba (Raila Odinga) ya Uenyekiti wa Tume ya AC. Hata hivyo, kama kiongozi kijana nchini Kenya, baada ya kukulia katika umaskini, najua maana ya kukosa,” alisema Owino.
"Kama Babu Owino, ninasimamia jamii ya kidemokrasia ambapo mtoto nchini Kenya atapokea dawa zinazofaa, na elimu na atapata kazi sawa. Vile vile, mtoto wa Uganda anapaswa kupokea matibabu sawa na ya mtoto nchini Kenya,”
Hata hivyo, Museveni aliongeza katika hotuba yake kuwa hakuwa na shaka kwa uongozi wa Raila Odinga na kuwa ushawishi wa Babu Owino ni mdogo usioathiri uwezo wa Rais Odonga kutekeleza majukumu yake.
Babu Owino amekuwa na uhusiano wa karibu na wa muda mrefu na kiongozi huyo wa upinzani Bobby Wine.
Rais Museveni ameiongoza Uganda kwa zaidi ya miongo mitatu huku akishutumiwa kukandamiza upinzani.