Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Video iliyosambaa hivi karibuni, ikimuonesha Simba akikatiza kwenye makazi ya watu huko Nairobi nchini Kenya, imezidi kuibua hufo kuhusu migogoro kati ya binadamu na wanyama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Picha hizo zilimnasana 'Mfalme huyo wa nyika' akipanda kwenye ukuta wa makazi ya watu, akamkata mbwa na kutokomea naye.
Matukio ya aina hii yaanzidi kuwa ya kawaida kote Afrika Mashariki, ambapo mashambulizi ya kulipiza kisasi yamesababisha mauaji ya wanyama pori.
Mbinu hafifu
Wataalamu wa wanyamapori wameonya kuwa hatua za muda mfupi zinazochukuliwa kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori huenda zisiwe suluhu za kudumu.
"Tunahitaji suluhu za muda mrefu kama vile kutengeneza shoroba za tembo na kuja na mipango endelevu ya matumizi ya ardhi," anasema Profesa Noah Sitati kutoka Shirika la WWF.
Kulingana na mtaalamu huyo, ni rahisi kwa tembo kuvamia mashamba ya mahindi kutokana na virutubisho wanavyokutana navyo katika zao hilo.
"Hili lisingejitokeza kama tungekuwa tumebainisha shoroba hizo," anaeleza.
Sitati anasema kuwa Tanzania imeandaa mpango kazi maalumu wa kushughulikia shoroba za wanyamapori na mapito mengine ya wanyama hao.
"Migogoro kati ya binadamu na wanyamapori bado ni tatizo kubwa na nina matumaini kwamba kuanzishwa kwa mpango kama huo kutaleta matokeo chanya," anasema.
Kuweka alama muhimu
Wakati Tanzania imerasimisha mpango huo, majirani zake wa Afrika Mashariki bado hawajafanya hivyo. Tanzania imefanikisha hilo kupitia uchoraji wa ramani na uwekaji wa miale, shughuli iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa WWF, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuanzisha miongozo ya uhusiano kati ya wanyama mbalimbali na makazi kupitia njia za uhamaji.
Hata hivyo, anatoa msisitizo kwenye mapitio ya miongozo hiyo ili iendane na mahitaji halisi.
“Kuna haja pia ya kuweka uzio kwenye maeneo hayo,” anaeleza.
Kenya imefanikiwa kuzungushia uzio kwenye baadhi ya hifadhi zake. Tanzania inakadiriwa kuwa na shoroba 62 za wanyamapori.
Chaguo gumu
Hifadhi ya taifa ya Shimba Hills ya nchini Kenya ilipolemewa na idadi kubwa ya wanyama pori, mamlaka ya wanyamapori nchini humo iliona ni jambo la busara kuanza kuwahamisha baadhi ya wanyama kuelekea hifadhi ya Tsavo Mashariki.
Zoezi hilo, lilishuhudia jumla ya tembo 150 wakihamishwa.
“Lilikuwa ni zoezi gumu na lenye gharama kwani lilihusisha helikopta na kuwachoma wanyamapori dawa za usingizi; na matokeo yake, baadhi ya tembo waliishia kupotea,” anaeleza Profesa Sitati.
Hali kama hiyo pia ilishuhudiwa katika Hifadhi ya Maasai Mara.
Tishio kubwa
John Noronha, Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (Usaid) anabainisha kuwa mamba na viboko ndio wanyamapori wanaohusika kwa kiasi kikubwa na migogoro ya aina hiyo nchini Tanzania.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa wanyama hao wamesababisha majeruhi 642.
"Kutegemeana kati ya binadamu na wanyamapori ni kipaumbele cha kitaifa kwa maendeleo endelevu na uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania, hata hivyo una matatizo yake," anasema.
Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migogoro ya Binadamu - Wanyamapori (2020 - 2024), unahusisha migogoro hiyo na upangaji duni wa matumizi ya ardhi.
Unadai kuwa mipango ya matumizi ya ardhi imetekelezwa bila kuzingatia hatari ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.