Mahakama ya Juu nchini Uganda imeamua kwamba mahakama za kijeshi nchini humo hazina mamlaka ya kisheria na haziwezi kuhukumu kwa haki katika kesi za kiraia.
Hukumu hiyo ilitolewa na Majaji Monica Mugenyi, Catherine Bamugemereire, Elizabeth Musoke, na Percy Night Tuhaise, ambao waliamua kuwa Mahakama Kuu ya kijeshi haina uwezo wa kushughulikia masuala ya mahakama zingine.
Jaji Bamugemereire alisisitiza umuhimu wa Mahakama Kuu ya Kijeshi katika masuala ya nidhamu ya kijeshi lakini akaeleza kuwa shughuli zake zinatakiwa kusitishwa,isipokuwa kwa kesi zinazohusisha masuala ya kinidhamu kwa maafisa wanaohudumu.
Bamugemereire katika uamuzi wake, amesitisha kesi zote zinazoendelea katika Mahakama hiyo ambayo huendeshwa na wanajeshi.
Ametoa wito wa kufanyiwa marekebisho kwa sheria ya jeshi la Uganda, UPDF akipendekeza kwamba mwanajeshi yeyote anayefanya uhalifu dhidi ya raia anatakiwa kufikishwa katika mahakama za kiraia.
" Pale ambapo mahakama ya kijeshi inaona kesi iko nje ya uwezo wake wa kisheria, itapeleka jalada la kesi la mshtakiwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili kuchukua hatua ya kumshtaki katika mahakama ya raia," Jaji Mkuu Musoke alisema.
Uamuzi huu wa kihistoria unasisitiza kanuni kwamba kesi za kiraia zinatakiwa kusimamiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika mahakama huru za kiraia.
Jaji Persy Night Tuhaise anapendekeza mashtaka yote ya makosa ya jinai yafanywe na DPP. Anadai kuwa haki lazima ionekane kutendeka.
" Mahakama Kuu ya Kijeshi ina ukomo wa kusikiliza masuala ya wanajeshi na ina mapungufu kama vile ukosefu wa uhuru na ukosefu wa mafunzo ya mahakimu wake katika masuala ya kisheria." Jaji Elizabeth Musoke alisema.
Mahakama ya kijeshi imeshutumiwa na mashirika mbalimbali na upande wa upinzani nchini humo kama chombo cha kuwakandamiza wanaopinga seriklai .
Mgombea urais mara nne wa Uganda Kizza Besigye ameshtakiwa katika mahakama hiyo.
Kanali huyo mstaafu wa jeshi mwenye umri wa miaka 68 ameshtakiwa kwa kumiliki silaha na makosa mengine katika mahakama ya kijeshi.
Mwaka wa 2018 Robert Kyagulanyi kiongozi wa chama cha upinzani cha National Unity Party, NUP pia alifikishwa katika mahakama hii ambapo alishtakiwa kwa uhaini,
Alikabiliwa na shtaka la kuwa na silaha kinyume na katiba lakini akaachiliwa baadaye.