Wazir wa Mambo ya Nje wa zamani wa Madagascar, Richard Randriamandrato. Picha: AU

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Madagascar inawania nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Mpeperushaji bendera wa nchi hiyo ni waziri wake wa zamani wa Mambo ya Nje, Richard Randriamandrato.

"Ugombeaji huu unaonyesha nia ya Madagascar ya kuchangia kikamilifu mustakabali wa bara letu, kwa kuzingatia umoja na utangamano wa kikanda," alisema rais wa Madagascar Andry Rajoelina mnamo Disemba 2024, alipokuwa akimtambulisha rasmi mgombea wa nchi hiyo.

Viongozi wa nchi na serikali za Afrika watamchagua mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika watakapokutana kwa mkutano wao wa kawaida mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 15 hadi 16 Februari 2025.

Randriamandrato anayezungumza lugha ya Kiingereza na Kifaransa kwa ufasaha, alihudumu kama Waziri wa Uchumi na Fedha kutoka 2019 hadi 2021.

Kisha akachukua nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia Machi hadi Oktoba 2022.

Ana miaka 65 ( alizaliwa 7 Machi 1959).

Kenya, Djibouti and Madagascar zinagombea nafasi za uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika/ picha AU 

Mnamo mwaka wa 2022 alifutwa kazi kwa amri ya rais baada ya kupiga kura kuunga mkono azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililolaani hatua ya Urusi kutwaa maeneo manne ya mashariki mwa Ukraine.

Hapo awali alifanya kazi kama mshauri maalum wa masuala ya kimataifa katika ofisi ya Waziri Mkuu na mshauri wa Rais wa masuala ya kimataifa.

Mtazamo wa bara

Randriamandrato anaamini kuwa Umoja wa Afrika na taasisi zake muhimu lazima uimarishe nafasi ya Afrika duniani.

"Kuwepo kwa amani kati ya nchi zinazopakana na zilizo katika vita kunahitaji kuendelezwa kwa njia ya mazungumzo na diplomasia," Randriamandrato anasema.

AU imeamua kufanya mageuzi ya utendakazi wake ambayo yatazingatia vipaumbele vichache na kufanya AU kuwa yenye ufanisi zaidi, kutoa huduma kwa raia wa Afrika bora zaidi na kupunguza kutegemea zaidi wadau wa maendeleo.

Randriamandrato mtaalamu wa siasa za kimataifa anasema “mageuzi yanahitaji idhini ya wakuu wa nchi ambao ndio chombo kikuu cha mamlaka. Na ni muhimu kwamba mageuzi haya yaidhinishwe inavyotakiwa kwa maafikiano ili kutoa mwelekeo kwa hatua zitakazochukuliwa baadaye.”

Ameeleza imani yake kwa Rais wa Kenya William Ruto ambaye ameteuliwa na AU kusimamia utekelezaji wa mageuzi hayo.

"Ninaamini mwaka 2025 Rais wa Kenya William Ruto ataleta mtazamo wa kipekee wa kuimarisha Muungano wa Afrika na Jumuiya yetu," Randriamandrato alisema alipokuwa akielezea maono yake kwa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama.

Anaunga mkono Umoja wa Afrika unaojitegemea zaidi ambao unaongozwa na ufadhili zaidi wa ndani wa shughuli za bara hilo.

Dira yake pia inaelekeza kwenye utekelezaji wa Eneo Huria la Biashara la Afrika ili kusaidia nchi za Afrika kufanya biashara zaidi ndani ya bara lao.

Changamoto kubwa zaidi

Madagascar ni kisiwa kilicho karibu na pwani ya kusini mashariki mwa Afrika. Ni kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani baada ya Greenland, New Guinea, na Borneo.

Rais wake Andry Rajoelina anasema jimbo la kisiwa lenye wakazi zaidi ya milioni 28 "liko tayari kukabiliana na changamoto hii" ya kuongoza taasisi zinazotekeleza mipango iliyoamuliwa na mataifa 55 ya Umoja wa Afrika.

Rafaravavitafika Rasata, Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar alisema "hii ni mara ya kwanza kwa Madagascar kuwa na mgombea wa nafasi hiyo ya juu ndani ya Tume ya Umoja wa Afrika."

Katika kinyang'anyiro hicho pia ni Kenya kupitia Waziri wake Mkuu wa zamani Raila Odinga na mgombea kutoka Djibouti ni Waziri wake wa Mambo ya Nje Mahamoud Ali Youssouf ambao wanawania nafasi hii mahsusi ikiwalenga viongozi wa Mashariki mwa Afrika.

Mmoja wao atachukua uongozi kutoka kwa Moussa Faki Mahamat wa Chad ambaye amekuwa Mwenyekiti kwa mihula miwili ya miaka 4 kila mmoja.

Madagascar inasema ugombea wa Randriamandrato, ambao ni wa kwanza kwa nchi hiyo, pia unawakilisha fursa ya kipekee kwa visiwa vya Bahari ya Hindi na kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kupaza sauti yao katika suala la umoja.

TRT Afrika