Raia wanachota maji kutoka Ziwa Kivu baada ya mji huo kuchukuliwa na waasi wa M23, huko Goma / Picha: Reuters

Shirika la afya la Afrika siku ya Alhamisi liliibua wasiwasi kuhusu kuhama kwa watu milioni moja katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC .

“Kuna hitaji la dharura la kushughulikia mzozo wa Goma. Kuhama kwa zaidi ya watu milioni moja huko Goma kunaleta changamoto kubwa kwa afya za watu kitaifa na kikanda," Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa-CDC), alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

Alitoa wito wa kudumisha utulivu ulioonekana huko Goma siku ya Alhamisi ili kurejesha utoaji wa huduma muhimu za afya kwa watu waliokimbia makazi yao, ufuatiliaji wa magonjwa na chanjo kwa walio hatarini.

Kulingana na Kaseya, wafanyakazi 200 wa CDC wa Afrika wako tayari kutoa misaada ya afya huko Goma.

Amesema kurejea kwa hali ya kawaida na usalama ni muhimu katika kuzuia milipuko ya magonjwa ambayo yanaweza kukumba mataifa mengine katika kanda hiyo.

Maelfu ya watu waliokimbia makazi yao

M23 ilianzisha mashambulizi makubwa wiki iliyopita katika mji wa Goma, ambao ni makazi ya watu takriban milioni 3.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hata hivyo, iliilaumu Kigali kwa kutuma wanajeshi wa Rwanda katika mji huo kusaidia waasi.

Wakati Rwanda ikikanusha kuwaunga mkono waasi, viongozi wa eneo hilo wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano huku watu kadhaa wakiuawa na mamia wengine kujeruhiwa.

Bado haijafahamika ni nani anayedhibiti jiji hilo pamoja na taasisi za serikali huko Goma ambayo inapakana na Rwanda.

Maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao, wengi wao wakikimbilia Rwanda, wakiwemo wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa kama vile UN na Benki ya Dunia.

Rwanda imesema raia wake tisa walifariki kutokana na moto unaodaiwa kuwaka kuanzia Goma hadi upande wa pili wa mpakani. Wanajeshi wa kulinda amani wasiopungua 17 pia wameuawa tangu wiki iliyopita.

TRT Afrika