Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa tangazo la kutafuta mawakili wa kumtetea kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Lord's Resistance Army (LRA), Joseph Kony.
Kwa mujibu wa tangazo lililochapishwa kwenye tovuti ya Mahakama hiyo, mawakili walio tayari kumtetea Kony wanapaswa kutuma maombi yao kwenye mahakama hiyo inayopatikana The Hague nchini Uholanzi, kabla ya tarehe 16 Mei, mwaka 2024.
Hati ya kukamatwa kwa Kony, mwanzilishi wa kundi la waasi la LRA, ilitolewa mwaka 2005, akiwa anakabiliwa na mashtaka 33 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu, yanayohusisha mauaji, kuteka watu nyara, ubakaji na kushambulia raia.
Kundi la LRA, likiongozwa na Kony, lilishambulia raia wa kaskazini mwa Uganda kwa karibu miaka 20 huku likipigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni.