Bill Gates na Rais wa Kenya William Ruto. Picha kutoka ukurasa wa X wa Rais Ruto

Mahakama Kuu imetoa maagizo ya kusimamisha hadhi ambayo taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation ilipewa na Serikali ya Kenya.

Mahakama imesimamisha hadhi hiyo ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini Kenya.

Serikali ilitangaza, kupitia Notisi ya Gazeti lake la tarehe 4 Oktoba 2024, kwamba taasisi Bill and Melinda Gates Foundation ingefurahia hadhi na haki maalumu, ikiwemo kinga fulani nchini.

Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye pia alitoa maagizo ya kuwazuia wafanyakazi wa shirika hilo kutofurahia marupurupu yoyote yanayoambatana na kinga au hadhi hiyo maalumu.

Hatua ya serikali kuipa kinga taasisi hiyo nchini, imepingwa na chombo cha Wanasheria, yaani Law Society of Kenya.

Zaidi ya hayo, Mahakama iliagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Sheria ya Nchi, kukusanya na kuhifadhi hati zote kuhusu mapendeleo hayo yaliyotolewa kwa Gates Foundation, ikiwa ni pamoja na maelezo ya makubaliano ya ushirikiano. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Februari 5, 2025, kabla ya kupangwa tarehe ya kusikilizwa .

TRT Afrika