Zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha na magari kusombwa na maji kufuatia mvua za El Nino nchini Kenya. / Picha: Reuters  

Rais wa Kenya, William Ruto ametuma jeshi kuongeza kasi ya uokoaji katika maeneo yaliyokumbwa na maafa ya El Nino nchini humo, huku idadi ya vifo ikifikia 171.

Mvua za msimu za El Nino, zimeharibu miondombinu kwenye taifa hilo.

Maafa hayo yameua karibu wanakijiji 50 wakiwemo watoto, baada ya kupasuka kwa bwawa katika eneo la Bonde la Ufa siku ya Jumatatu.

Mkasa huo ulioukumba kijiji cha Kamuchiri, katika kaunti ya Nakuru, unatajwa kuwa tukio baya zaidi nchini Kenya tangu kuanza kwa msimu wa mvua za mwezi Machi na Mei.

Makataa ya saa 48

Ruto, ambaye aliwatembelea waathirika wa mafuriko ya Kamuchiri baada ya kuongoza kikao cha baraza la mawaziri jijini Nairobi, alisema serikali yake imechora ramani ya vitongoji vilivyo hatarini kukumbwa na mafuriko.

"Jeshi limeshaandaliwa pamoja na vijana na vyombo vyote vya usalama kusaidia wananchi katika maeneo kama hayo kuhama ili kuepuka hatari zozote za kupoteza maisha," alisema Jumanne.

Kulingana na Rais Ruto, watu wanaoishi maeneo yaliyoathiriwa wamepewa saa kuhama.

Bora nusu shari

"Sio wakati wa kubahatisha, bora nusu shari kuliko shari yenyewe."

Maafa ya Kamuchiri - ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 48 - na kuharibu barabara, kung'oa miti, nyumba pamoja na magari.

Takriban watu 26 walilazwa hospitalini, Ruto alisema, huku akihofia kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea.

Baraza la mawaziri nchini Kenya limeonya kwamba mabwawa mawili ya Masinga na Kiambere yote yaliyo chini ya kilomita 200 kaskazini mashariki mwa mji mkuu "yamefikia miinuko ya kihistoria", na hivyo kuashiria maafa kwa wale walio chini ya mto huo.

'Kuhamishwa kwa nguvu'

"Wakati serikali inahimiza uhamishaji wa hiari, wale wote ambao wamesalia ndani ya maeneo yaliyoathiriwa na agizo hilo watahamishwa kwa nguvu kwa masilahi ya usalama wao," ilisema taarifa hiyo.

Mkasa huo wa Jumatatu unakuja miaka sita baada ya ajali ya bwawa la Solai, pia katika Kaunti ya Nakuru, kuua watu 48, na kusababisha mamilioni ya lita za maji yenye matope kupenya kwenye nyumba na kuharibu miundombinu ya umeme.

Maafa ya Mei 2018 yaliyohusisha hifadhi ya kibinafsi kwenye shamba la kahawa pia yalifuatia wiki za mvua kubwa iliyosababisha mafuriko mabaya na maporomoko ya matope.

Wanasiasa wa upinzani na makundi ya watetezi wameishutumu serikali ya Ruto kwa kuchelewa kuchukua hatua za haraka licha ya kutolewa kwa tahadhari ya hali ya hewa.

'Kutokujiandaa'

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga alisema Jumanne mamlaka zilishindwa kufanya "mipango ya dharura" kukabiliana na hali mbaya ya hewa.

"Serikali imekuwa ikizungumza sana juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, lakini hali ni tofauti panapotokea majanga," alisema.

"Tumebakia kupanga tu."

Waziri wa Mazingira Soipan Tuya aliwaambia wanahabari jijini Nairobi kwamba serikali inaongeza juhudi za kujitayarisha vyema kwa matukio hayo.

Uharibu mkubwa

"Tunaendelea kuzingatia hitaji la kuwekeza katika mifumo ya hadhari ya mapema ambayo huandaa idadi ya watu, siku, wiki na miezi kabla ya hali mbaya ya hali ya hewa, kama vile mvua kubwa tunayopata."

Jumuiya ya kimataifa, ikiongozwa na Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, imetuma salamu za rambirambi kwa familia zilizoathiriwa.

Hali mbaya hiyo ya hewa imesababisha uharibifu mkubwa katika nchi ya jirani ya Tanzania ambapo zaidi ya watu 100 wanaripotiwa kupoteza maisha.

Mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya watu 300 walikufa kutokana na mvua na mafuriko nchini Kenya, Somalia na Ethiopia.

TRT Afrika