Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Serikali ya Tanzania imeanza maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Nchi hiyo, kutoka Afrika Mashariki inatarajiwa kuandaa mashindano hayo makubwa na yenye hadhi barani Afrika, kwa kushirikiana na majirani zao wa Kenya na Uganda, michuano ambayo itaanza Juni 2027.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Tanzania iliikabidhi kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) kutoka China, eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 14.57, kwa ajili ya ujenzi huo wa uwanja wa kisasa.
Uwanja huo utajengwa katika eneo la Olmoti, ndani ya jiji hilo ambalo ni kitovu cha utalli nchini Tanzania.
Uwanja huo, ambao unagharimu Shilingi bilioni 286 za Kitanzania, umepewa jina la Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, na utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji waliokaa 30,000.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amesema ujenzi wa uwanja huo ni hatua muhimu katika maandalizi ya michuano hiyo, miaka 20 baada ya uwanja mwingine wa kisasa wa Benjamin Mkapa katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
"Hiki ni kitu kizuri kwa Tanzania wakati tunajiandaa kuandaa AFCON 2027, uwekezaji huu utaipa nchi yetu taswira nzuri kimataifa," amesema Ndumbaro.
Meneja mradi huo, Gao Hongchun amesema kuwa mkandarasi huyo atahakikisha kuwa anajenga uwanja wa kisasa zaidi barani Afrika.
Ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 22 ijayo, kulingana na Honhchun.
Mwezi Machi mwaka huu, kampuni ya CRCEG ilitiliana saini na serikali ya Tanzania kuanza kwa ujenzi wa uwanja huo, jijini Arusha.