Mkutano wa COP29 wa dunia wa kujadili athari za mabadiliko ya tabia nchi umekamilika nchini Azerbaijan huku nchi nyingi hasa zinazoendelea zikiwa hazijaridhishwa na matokeo yake.
Nchi zenye kipato kikubwa ziliahidi kuchangia hadi dola bilioni 300 kila mwaka ifikapo 2035 kwa ajili ya mikakati ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi kwa nchi zinazoendelea.
Pia ziliahidi kufanya kazi pamoja ili kuongeza fedha kwa nchi zinazoendelea, kutoka vyanzo vya umma na vyanzo binafsi, hadi kiasi cha dola trilioni 1.3 kwa mwaka ifikapo 2035.
Mataifa yanayoendelea ambayo yalikuwa yanataka mchango wa zaidi ya dola trilioni 1 yaliyaita makubaliano hayo kuwa ni duni na kwamba sio rasilimali muhimu walizohitaji kushughulikia ugumu wa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Lakini kwa nini malalamiko haya?
Nchi zinazoendelea zinachangia pakubwa kuchafua hewa. Kwa mfano Ulaya Magharibi na Marekani, ambazo zinafurahia baadhi ya viwango vya juu zaidi vya ustawi, zinawajibika kwa zaidi ya 45% ya gesi chafu hasa kutoka viwanda vyake.
Hewa imechafuliwa kupitia kuchoma nishati ya mafuta, makaa ya mawe au gesi, ambayo hutoa kaboni dioksidi.
Uchomaji wa mafuta ili kuzalisha nishati ya kutengeneza vitu kama vile saruji, chuma, vifaa vya elektroniki, plastiki, nguo na bidhaa nyenginezo imechangia hatari. Kukata misitu ili kuunda mashamba ya malisho.
Magari mengi ya mizigo, meli na ndege hutumia nishati ya mafuta. Hiyo inafanya sekta ya usafiri kuwa mchangiaji mkuu wa gesi chafu.
Kwa upande mwengine nchi zenye kipato kidogo zinaumia kutokana na athari kubwa ya hewa chafu ilhali nchi hizo hazichangii pakubwa katika uchafuzi wa mazingira.
Kwa mfano Afrika inachangia kati ya asilimia 3 na 4 tu ya gesi chafu duniani ilhali ni bara ambalo lina uwezo mdogo zaidi wa kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa.
Mawimbi ya joto, mvua kubwa, mafuriko, vimbunga vya kitropiki na ukame wa muda mrefu vina athari mbaya kwa jamii na uchumi, na kuongezeka kwa idadi ya watu walio hatarini.
Mnamo 2009, nchi za kipato cha juu zilizo na mchango mkubwa wa kihistoria katika mabadiliko ya hali ya hewa zilikubali kuwajibika na kujitolea kukusanya dola bilioni 100 kila mwaka ifikapo 2020 ili kufadhili hatua ya hali ya hewa katika nchi za kipato cha chini.
Hata hivyo, ahadi hiyo haikutimia na hata ufadhili zaidi unahitajika ili kuendeleza hewa safi na kuimarisha ustahimilivu katika nchi zinazoendelea.
Mwaka 2015 nchi 196 zilikutana nchini ufaransa 2015 na kukubaliana kuwa ni muhimu kuweka viwango vya ongezeko la wastani wa hali joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 2.
Lakini hii ingehitaji rasilimali zaidi. Hii inahitaji miradi tofauti kwa nchi binafsi zinazoathiriwa zaidi ili kujikinga na hewa chafu.
Na hii ndiyo sababu nchi zilizoendela katika mkutano uliokamilika wa COP29 Azerbaijan zimesema nchi za kipato kikubwa zimegoma kutoa fedha zaidi ili kuwasaidia haraka, kwani tayari utafiti unaonyesha kuwa hali joto ya duniani imeshapita nyuzi joto 3 kiashiria kwamba athari za mabadilio ya tabia nchi zinaendelea kuongezeka.