Hindou anasema alizaliwa kwa sababu ya upendo wake kwa mazingira. Picha: TRT Afrika     

Na Firmain Eric Mbadinga

Hakuna kitu cha muhimu maishani kama kutambua kusudi lako hapa duniani. Hiyo ndiyo imani ya Hindou Oumarou Ibrahim.

"Nilikuja hapa duniani kwa dhumuni moja tu; upendo kwa mazingira na sijawahi kufikiria kujizuia kutekeleza hilo," anasema.

Akiwa amezaliwa Chad, ametokea kwenye familia ya kawaida sana hadi kuwa mwanaharakati wa mazingira anayetambulika kimataifa huku kazi yake ya uanajiografia ikiwa imechochewa na uthubutu wake, moyo wa kujitoa kwa jamii na dhamira yake maishani.

Maisha yake utotoni aliitumia zaidi mjini N'Djamena, huku muda wake wa likizo akiutumia na wakazi wa Mbororo, akishiriki nao kuchunga ng'ombe.

Ukaribu wake na watu wa Mbororo, pamoja na changamoto alizopitia kama mwanamke, viliamsha ndani yake, ari ya kuwa mwanaharakati wa mazingira katika jamii yake.

Hindou amepata bahati ya kuizunguka dunia, kutoka mkutano wa COP 15 nchini Ufaransa ambapo alisaini kwenye mkataba wa Paris kwa niaba ya watu wa asili na mkutano wa mazingira uliofanyika New York mwaka 2019, pamoja na ule wa COP 28 uliofanyika Dubai, mwaka jana.

Upole wake unaoambatana na uelewa wa masuala mbalimbali, ndivyo vinavyomuweka katika nafasi nzuri ya kufanya uanaharakati zaidi."Lazima tulinde mazingira ambayo yanatuendeleza. Maisha yetu, na mfumo wetu wa maisha, unategemea mazingira," anasema.

"Kampeni ya ulinzi wa mazingira ni jambo la kawaida kwangu," anasema Hindou ambaye hujulikana sana kwa mavazi yake Kiafrika, mahali popote anapokwenda.

Bidii ya Kampeni

Hindou amejifunza sifa ya uwajibikaji toka akiwa shuleni na ni tunu anayoiamini na kuitumia kwa ajili ya jamii na nchi yake.

"Nilipokuwa shule ya msingi, nilitamani sana kuzungumza kuhusu haki zangu kama mtoto wa kike kutoka kabila la Fulani," anaikumbusha TRT Afrika.

Hindou anatokea katika jamii ya wafugaji ya Mbororo./Picha:TRTAfrika

"Hapo ndipo nilipokuja kuelewa kuwa huwezi kuzungumzia haki za binadamu bila kugusia mazingira na ulinzi wake, na nikaamua kuanzisha Chama cha Wanawake wa Asili na Watu wa Chad (AFPAT)," anasema Hindou, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Pritzker Emerging Environmental Genius ya mwaka 2019.

Ilikuwa ni mwaka 1999, wakati Hindou ana miaka 15 tu. Mpango wake ukaanza kuzaa matunda na kwenda zaidi ya nyanda za kusini-magharibi mwa Chad kupitia utetezi na uhamasishaji.

Mbali na tuzo ya Pritzkerm Hindou alipata tuzo nyingine ya Holbrooke 2020, aliyopewa ijulikanayo kama Refugees International and the Danielle Mitterrand Prize. Mojawapo ya mafanikio muhimu ya Hindou kama mwanajiografia ni mchango wake katika kubuni ramani shirikishi ya 2D na 3D katika ukanda wa Saheli.

Mradi huo, unaotekelezwa kwa ushirikiano na UNESCO, unalenga kuweka mipaka ya maeneo yanayokaliwa na jamii tofauti, kwa kuzingatia upekee wa mifumo yao ya ikolojia. Lengo lingine la uchoraji ramani wa pande nyingi ni kukabiliana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika eneo hili.

Mpango huo pia unazingatia maarifa ya watu wa kiasili kuhusu asili kama sehemu ya msukumo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ushirikiano kati ya Hindou na UNESCO umepelekea kutambuliwa kwa umiliki wa ardhi kwa wanawake wa nchini Chad na hivyo kuunda shughuli za kuzalisha kipato kwa kuzingatia kilimo cha ikolojia ya maeneo maalum. Juhudi zake thabiti pia zilisababisha kuanzishwa, katika COP15 huko Paris, hadidu rejea tano muhimu kwa watu wa kiasili, ikijumuisha haki zao na maarifa.

Changomoto za kifedha

Mwanzo wa harakati za Hindou ulikuwa mgumu, hasa kutokana na uhaba wa fedha. "Harakati zangu za awali hazikutegemea pesa zozote kutoka kwa wafadhili," anakumbuka.

Hindou alihofia athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa jamii za kiasili./Picha:TRTAfrika

"Nililipwa pesa za kujikimu kupitia mikutano na matukio ya kimataifa, nilihakikisha nakula chakula cha bei rahisi kabisa na kukaa kwenye hoteli za kawaida."

Hindou alifanikiwa kuendesha harakati zake kupitia fedha za akiba alizojiwekea. "Nilikuwa nategema vyanzo hivyo ili kulinda vitu ninavyovipenda," anaiambia TRT Afrika.

Pamoja na mafanikio hayo, Hindou anaona kama hajafika pale anapopataka. Takwimu zinadhihirisha ukubwa wa kazi yake.

Harakati ngumu

Takribani hekta 200,000 za misitu zimepotea nchini Chad, kutokana na ukataji wa miti, kulingana na Shirika la France Nature Environment. Hali hii, inazidisha kasi ya kuenea kwa jangwa katika ukanda wa Saheli.

Jangwa hilo linakadiriwa kuendelea kwa kasi ya kilomita tatu kila mwaka. Taarifa hizi, japo si rasmi, zinampa Hindou ari ya kusaidia kudumisha usawa katika mifumo ya ikolojia.

“Ili kulinda mazingira, ni lazima kwanza tutambue viumbe vyote katika maumbile, si binadamu tu, bali pia mimea na wanyama,” anasema.

"Tunatakiwa kulinda ndege, wadudu, mimea, miti na nyasi, vyote hivyo vina thamani na haki. Mifumo yote ya ikolojia imeunganishwa; mifumo ikolojia yote inategemeana; tukiharibu moja, ina maana tunaharibu usawa wa mwingine."

Hata katika mikutano ya kimataifa kama vile COP28, Hindou ametoa maoni kuhusu maendeleo ya mipango kupitia hati zilizotafsiriwa katika lugha za ndani.

Hindou akiwa katika harakati zake.

Vionjo vya mkutano huo vinaonesha imani yake katika kushirikisha wadau ili wawe kwenye mstari mmoja, ambayo ni hatua muhimu katika harakati zake.

"Sote tulikuwa tumechoka na tulikuwa tumekusanyika pamoja, ndipo mmoja wetu akaniambia, 'Tunajua unachofanya. Tunakuunga mkono kwa njia zote'.

"Kauli hiyo ilinipa motisha sana, Msaada wa hali ni muhimu sana kama ulivyo wa mali," anasema.

"Nimedhamiria kupambana dhidi ya gesi chafu na zilizojaa sumu zenye kuongeza hali joto duniania," anasema Hindou

TRT Afrika