Baraza la Kimataifa la Utalii linakutana katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali. Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika barani Afrika.
Mkutano huu unajumuisha wadau katika sekta ya utalii duniani ambao nia yao ni kujenga rasilimali tofauti katika sekta hiyo.
"Afrika inapaswa kusimulia hadithi yake yenyewe kwa njia yake na kuweka simulizi chanya kuhusu Afrika. Hatuwezi kumudu kuendelea kukaa kimya katika zama hizi za habari za uongo. Tunapaswa kusimama na kuweka rekodi sawa. Afrika sio tu ya siku zijazo, ni sasa,” rais wa Tanzania Suluhu Samia Hassan alisema.
Rais Samia amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa Afrika lazima ijiulize maswali mazito ili utalii upige hatua zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na kuweka masoko ya kimkakati na chapa, utafiti na uhifadhi.
Mkutano huo unafanyika nchini Rwanda, ambayo imewekeza vikubwa katika sekta ya utalii.
Duniani sekta ya utalii na usafiri imeibuka, lakini usafiri ndani ya nchi za Afrika umekuwa mgumu," amesema rais Paul Kagame wa Rwanda katika ufunguzi wa mkutano huo.
" Tuliibuka kuwa Rwanda ambayo mtu yeyote duniani angependa kuitembelea," rais Kagame alielezea akiashiria kuwa Rwanda inaendelea kuibuka kutoka katika changamoto zilizoletwa na mauaji ya kimbari, na imetumia utalii wa aina tofauti kuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji.
"Kila mwaka tunakaribisha wageni wengi sana kuja Rwanda na kufurahia uzuri wa asili wa kipekee, kuhudhuria matukio ya michezo au kushiriki katika mikusanyiko kama hii. Hii ni ishara kuwa hatuuchukulii utalii kwa mzaha," Kagame ameongezea.
Kama ilivyo kwengineko barani Afrika, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Tanzania, NBS inaonesha kuwa utalii una mchango mkubwa katika uchumi, unaochangia 17.2% ya pato la taifa la Tanzania na 25% ya mapato ya fedha za kigeni.
Rais Samia alisema Afrika inapaswa kuweka kipaumbele katika uhifadhi na kuunga mkono juhudi za kuhifadhi maeneo ya kitamaduni, vitu vya kale na mila kwa ajili ya vizazi vijavyo ikiwa bara hilo linataka kuendelea kutegemea vivutio vya asili.