Na Ovigwe Eguegu
Mtu yeyote anayefuatilia kwa umakini atatambua kuwa siasa zinazohusiana na mahusiano ya kimataifa zinabadilika.
Katika ulimwengu wa magharibi, Serikali za Amerika Kusini zinahama kutoka katika ushawishi wa kiuongozi wa Marekani. Barani Asia, Uchina inazidi kupanda katika umashuhuri kimataifa, na kwa kiwango kikubwa zaidi, ikihama kutoka katika ushawishi na uongozi wa mataifa ya Ulaya na kuelekea ulimwengu ambao nchi nyingi zina ushawishi sawia, zikiwa uhuru kujiamulia mambo yao wenyewe.
Katika muktadha huu, lengo ni kuelewa umuhimu wa Afrika katika maendeleo ya kimataifa, hasa jinsi Serikali za Afrika zinavyokabiliana na mabadiliko haya na nini kinapaswa kufanywa ili kujiweka katika nafasi zitakazoleta manufaa huko mbeleni.
Wachambuzi na watunga sera wanaamini kuwa Afrika inagombaniwa upya, na katika mbio hizi, kusudi la mataifa yenye nguvu duniani ni kupata madini muhimu yanayohitajika kwa ajili ya maendeleo na utengenezaji wa teknolojia ambayo inaipa nguvu kile kinachoitwa mapinduzi ya nne ya viwanda.
Marekani, kwa mfano, katika nyaraka zake kadhaa za sera imeangazia umuhimu wa kupata "madini ya kimkakati" ambayo yanapatikana kwa wingi barani Afrika kama vile kobalti, lithiamu na alumini.
Halikadhalika China, ambayo ina mahusiano ya kina ya kiuchumi na nchi mbalimbali za Afrika ambazo zimeufungulia mlango wazi uchumi wake mkubwa na nishati ya kutosha. Wote hawa ni washindani wa kiuchumi, lakini swali ni: Je, Serikali za Afrika zina nini cha kusema?
Zimbabwe kwa upande wake imeamua kuchakata madini yake ya kimkakati ndani ya nchi, kama vile chuma na platinamu. Nigeria imeainisha lithiamu kama madini ya kimkakati, na Guinea imepanga upya msimamo wake kuhusu jinsi ya kutumia rasilimali zake, kulinda maslahi ya taifa.
Huku kukiwa na mijadala kuhusu "kugombaniwa upya" kwa Afrika, ukweli ni kwamba Serikali za kigeni hazina uhuru wa unyonyaji wa kiholela, tofauti na chini ya Mkutano wa Berlin na kilele cha Vita Baridi.
Hali iliyopo sasa katika siasa za kimataifa ni kwamba Waafrika wana uvumilivu mdogo dhidi ya uharibifu wa mazingira, upotezwaji makazi na majanga mengine ambayo yalijitokeza katika karne ya 19 na 20 kwa kigezo cha uanzishwaji na ukuaji wa viwanda.
Kinyang'anyiro cha samaki, nishati
Nchi nyingi za Kiafrika sasa hivi zinajiweka nafasi ya mbele, huku zikitambua kwamba mfumo wa biashara na uchumi sasa ni wa kimataifa.
Siasa za kimataifa za wakati huu zinaonyesha kwamba Serikali za Afrika sasa ziko katika nafasi ya kujiamulia mustakabali wa uhusiano wa kimataifa, hii ikiwa na maana kwamba mifumo iliyotawala biashara na diplomasia kwa muda mrefu imepinduliwa. Mfano halisi ni kati ya Mali na Ufaransa.
Washington sasa inaongeza juhudi za kidiplomasia ili kupata uungwaji mkono katika bara hilo, huku Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken akifanya ziara katika nchi kadhaa za Afrika na kuzungumza juu ya hitaji la maendeleo ya rasilimali asilia na madini ya kimkakati katika maeneo ya Afrika yanayoongozwa na Marekani.
Makamu wa Rais Kamala Harris pia ametembelea Ghana, Tanzania na Zambia hivi karibuni kukutana na viongozi wa kisiasa na vijana ambapo alisema safari hiyo ilikusudia ''kwa kutambua kwamba mataifa ya Afrika ni muhimu kwa ustawi na usalama wa kimataifa - na mawazo na ubunifu wao utanufaisha ulimwengu. ''
China ina nafasi ya pekee katika suala hili, kwa kuwa Beijing imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa nchi za Afrika katika miaka ya hivi karibuni na imekuwa chaguo bora kwa viongozi wa Afrika wanaotafuta uhusiano mpya wa kiuchumi.
Zaidi ya hayo, Serikali za Afrika kama Burundi, Ethiopia na Niger sasa zinanufaika zaidi kutokana na kushuka kwa asilimia 98 ya ushuru wa bidhaa zinazosafirishwa kwenda China kama sehemu ya juhudi pana za Beijing kuongeza uagizaji bidhaa kutoka Afrika.
Tanzania na Uganda pia zilianza kunufaika kutokana na mauzo ya bidhaa kwenda China bila kutozwa ushuru. Huku ikiwa imepitisha sera inayojumuisha bidhaa zaidi ya 8,800, China inataka kuongeza uagizaji wa bidhaa kutoka Afrika hadi dola bilioni 300 ifikapo 2025.
Jambo la kuzingatia ni kwamba wakati mataifa yenye nguvu kama vile Marekani na China yanatafuta ushawishi wa kina baina yao na Serikali za Afrika, nchi za bara hilo zimejikuta zina uhuru katika kuchagua shirikiano zinaotaka, hasa wakati wa kuzingatia faida za kiuchumi zinazopatikana katika uhusiano wa Afrika na China.
Kuanzia mipango ya misamaha ya madeni hadi mauzo ya nje bila ushuru, Serikali za Kiafrika zina nafasi ya pekee katika kushawishi mataifa makubwa yenye nguvu na hivyo kuchagiza mabadiliko ya siasa za kimataifa zitazozalisha aidha taifa moja lenye nguvu au mataifa mengi yenye nguvu au mfumo wa kutofungamana na upande wowote.
Masuala ya bahari ni eneo lingine ambapo Afrika inaonyesha uwezo wa kushawishi duru za kimataifa.
Kwa kuzingatia njia kuu za meli kama vile Mfereji wa Suez karibu na Misri na Mlango-Bahari wa Bad-el Mandeb kwenye Pembe ya Afrika unaohudumia Ulaya na Asia kwa kupitisha mafuta na gesi asilia, nchi za Afrika zimesonga mbele katika kuboresha uwezo wake wa kukabiliana na matishio ya pamoja ya uharamia huku zikitumia uhuru wa kushughulikia maslahi ya nje.
Mbali na hayo, maliasili zinazozunguka maeneo kama Ghuba ya Guinea na Pembe ya Afrika pia zinagombaniwa na nchi nyingi kutokana na shughuli za uvuvi wa samaki, na vyanzo vya nishati kama gesi asilia.
Katika muktadha huu, iwapo kutakuwa na uratibu mzuri barani kote basi rasilimali za bahari ya Afrika zitaleta manufaa endelevu katika bara zima.
Yanayowezekana kwa Afrika
Sheria na Azimio la Yaounde (YCoC), kwa mfano, ilitiwa saini na mataifa 25 mwaka wa 2013 kwa ajili ya kuongeza ushirikiano katika upashanaji habari, kuzuia na uchunguzi - yote ili kukabiliana na matishio ya usalama wa baharini kama vile uharamia, magendo, uvuvi haramu na uchafuzi wa mazingira.
Ushirikiano wa aina hii, japo unasifiwa, lakini haujaleta matokeo yanayotarajiwa kwa sababu, kulingana na ripoti ya Chatham House, matukio ya utekaji nyara 130 kati ya 135 wa baharini yaliyotokea duniani kote yalifanyika katika Ghuba ya Guinea.
Lakini matokeo ya YCoC hayana vifungu vya kisheria vinavyolazimisha utekelezaji, pia kuna mapungufu kifedha na kiutendaji.
Muhimu zaidi, kwa vile Serikali za Afrika zimeanza kutekeleza mikakati mipya ya maendeleo ya uchumi, zinaweza kujikuta katika ushindani na mataifa yenye nguvu ukizingatia siasa za kimataifa zinaweza kuathiri uhusiano wa kimataifa wa baharini.
Kwa kuhitimisha, mabadiliko katika siasa za kimataifa, kama ilivyotajwa hapo juu, yanaonyesha dhahiri kwamba ulimwengu unaondoka katika uongozi wa Marekani kuelekea mfumo wa ushawishi mpana ambapo nchi za Asia, Amerika Kusini na Afrika zinapata sauti zaidi katika masuala ya kimataifa.
Hii imeleta fursa mpya kwa Afrika kwani Serikali mbalimbali ndani ya bara hili zinatekeleza majukumu mapya katika siasa za kimataifa kama vile kushawishi utaratibu kuhusu madini ya kimkakati na rasilimali nyingine kama hizo.
Ushawishi huu katika duru za kimataifa pia unaonekana ndani ya shughuli za jumuiya ya kimataifa kama vile kura za Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) na ukuaji wa ushirika mpya kama vile BRICS, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kando na maamuzi ya nchi Zisizofungamana na upande wowote.
Kwa kutafuta uwakilishi mkubwa zaidi katika Mataifa yanayostawi (G20) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ina maana Afrika inahama kutoka nafasi ya mtazamaji tu hadi kuwa mhusika hasa katika jukwaa la kimataifa.