Profesa Kithure Kindiki ameapishwa kuwa Naibu Rais baada ya wiki kadhaa za mvutano wa kisheria.
Awali Mahakama Kuu ya nchi hiyo ilisitisha kuapishwa kwa Kindiki baada ya Gachagua na jopo lake la mawakili kuwasilisha kesi zaidi ya 30 kuzuia kuondolewa kwake.
Hata hivyo, Mahakama iliondoa zuio hilo na kuruhusu kuapishwa kwa Kindiki.
Sherehe ya kuapishwa kwa Kindiki imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC), jijini Nairobi na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Kenya.
Gachagua alitimuliwa kutoka ofisini kwa mashtaka kadhaa yakiwemo ukiukaji mkubwa wa katiba na kuzua chuki za kikabila, shutuma ambazo amezikana na kusema zimechochewa kisiasa.Kabla ya uteuzi huu, Kindiki, mwenye umri wa miaka 52, alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa miaka miwili chini ya serikali ya Rais William Ruto.
Kufuatia mashaka yaliyomkumba Gachagua, huenda Kindiki amejifunza kitu kutoka kwa mtangulizi wake hivyo kumfanya kuwa Naibu Rais mwaminifu na mtiifu zaidi kwa bosi wake.
Mpaka sasa, haijafahamika, ni hatua gani za kisheria Gachagua atazichukua baada ya kuapishwa kwa Kindiki.