Rais wa Baraza la mpito, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, amerejea Sudan baada ya ziara rasmi ya siku moja nchini Uganda ambapo amefanya mazungumzo yaliyodumu saa moja na Rais Museveni.
Kiongozi wa Sudan na mwenyekiti wa baraza la mpito la nchi hiyo Abdel Fattah al Burhan amefanya mkutano na rais Yoweri Museveni nchini Uganda huku ziara hiyo ikiwa ni safari ya sita ya Jenerali huyo wa Sudan nje ya nchi hiyo tangu kuonekana hadharani kwa mara yake ya kwanza mwishoni mwa mwezi Agosti.
Kwa muda sasa, Al Burhan amekuwa akiendelea na safari za nje ya nchi ikiwa ni pamoja Na kufika Misri, Sudan Kusini na Uturuki miongoni mwa nchi nyingine huku vita vikiendelea huko Khartoum.
Kaimu Waziri wa Mambo ya nje, Balozi Ali Al-Sadiq amesema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara ya Rais A Burhan kwa nchi kadhaa jirani, zenye wasiwasi juu ya uharibifu na hujuma zinazoikabili Sudan.
Balozi Ali Al-Sadiq amebainisha kuwa marais hao wawili waligusia uhusiano kati ya Khartoum na Kampala na hali ya ndani ya Sudan, hasa miji ya Khartoum na Darfur.
Awali, kabla ya mkutano wa viongozi hao, Baraza kuu la Sudan liliandika siku ya jumamosi,kuwa Kamanda huyo mkuu wa Vikosi vya wanajeshi wa Sudan (SAF), Burhan atakutana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni Mjini Kampala, ambapo watajadili "uhusiano wa nchi hizo mbili na masuala muhimu."
Balozi Ali Al-Sadiq amemaliza kwa kusema kuwa Rais Museveni, wakati wa mkutano huo ameihakikishia Sudan uungwaji wa nchi yake kwa umoja wa Sudan, uadilifu wa eneo, na utulivu wa watu wake.
Nchi hiyo imekuwa ndani ya vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mapigano yalipozuka katika mji mkuu kati ya vikosi vya wanajeshi wa Sudan (SAF) linaloongozwa na Burhan na Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF vinavyosimamiwa na naibu wake aliyegeuka kuwa mpinzani Mohamed Hamdan Dagalo.
Kumekuwa na mapigano karibu na makao makuu ya kijeshi ya Khartoum ambapo Burhan alikuwa ameweka makao makuu kufikia mwezi uliopita kabla ya kushuhudia mapumziko mafupi ya wiki mbili na kuwaka tena, kupitia mashambulizi kutoka RSF, wakazi walisema.
Al Burhan amekuwa akiiongoza Sudan tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda Mrefu Omar al Bashir mnamo 2019 alipoteuliwa kuwa mkuu wa Baraza Kuu la Kijeshi na raia lililopewa jukumu la kuongoza utawala wa mpito hadi demokrasia kamili.
Angalau watu 7,500 wameuawa tangu mzozo huo ulipoanza Aprili 15, kulingana na makadirio yaliyotolewa na mradi wa Takwimu za eneo na tukio la mapigano ya Silaha Armed Conflict Location & Event Data.