Rais wa Kenya William Ruto, ameagiza kusitishwa kwa kandarasi ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa JKIA na ya nishati iliyopewa kampuni ya Adani kutoka India.
“Nilishawahi kusema huko nyuma, na narudia tena leo kwamba kutokana na ushahidi usio na shaka au taarifa za kuaminika kuhusu rushwa, sitositi kuchukua hatua madhubuti," Rais Ruto alisema.
" Naelekeza kwamba...wakala wa ununuzi ndani ya Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Uchukuzi. Nishati na Petroli zisitishe mara moja, mchakato unaoendelea wa shughuli ya upanuzi wa uwanja wa JKIA ambao ni ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na mkataba wa usambazaji wa njia za umeme wa kampuni ya KETRACO uliohitimishwa hivi karibuni na mara moja kuanza mchakato wa kuhusisha washiriki wengine," aliagiza.
Mwezi Julai 2024 Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KAA) ilithibitisha nia ya kampuni ya Adani kuhusishwa kwenye upanuzi wa uwanja wa ndege wa JKIA, licha ya kampuni hiyo kutopewa kandarasi yoyote .
Hatua hiyo, ilichochea maandamano kutoka kwa wananchi, wakioneshwa kutokufurahishwa na maamuzi hayo, wakidai kuwa serikali ilikuwa inapanga njama za kuuza uwanja huo wa ndege wa kimataifa.
Haya yanajiri kuhu mamlaka moja nchini Marekani ikimshtaki mmiliki wa Kampuni ya Adani Holdings Limited ya India, bilionea Gautam Adani na watendaji wengine saba kwa tuhuma za rushwa na ulaghai wa dhamana kwa majukumu yao katika mpango wa mabilioni ya dola ili kupata fedha kutoka kwa wawekezaji wa Marekani na taasisi za kifedha duniani.
Washitakiwa hao ni pamoja na Adani, Sagar Adani na Vneet Jaain, watendaji wa kampuni ya India ya nishati mbadala ya Indian Energy Company.
Mkataba kati ya kampuni ya Adani na Kenya wa usambazaji ya umeme unagharimu zaidi ya dola milioni 700 ambao pia ulikuwa umeidhinishwa na Wizara ya Nishati ya Kenya.
Oktoba mwaka huu, kampuni ya Adani Energy Solutions ilitia saini mkataba wa miaka 30, wa dola milioni 736 wa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi na Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya.
Mahakama nchini Kenya ilihairisha mkataba huo mwezi huo wa Oktoba.