Wafugaji hao 8 kutoka Kenya wamepewa miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria katika mahakama ya Kijeshi ya Uganda mwezi Aprili 2022. Picha : Bunge Kenya 

Wito huu kwa bunge unajiri huku masharti magumu yakiwekwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kabla majadiliano yoyote kuhusu msamaha kwa raia wa Kenya waliozuiliwa yafanyike.

Ripoti ya awali kuhusu kesi ya Wakenya hao iliyotoka kwa Waziri wa nchi za kigeni wa Kenya Dkt. Alfred Mutua iliwasilishwa mbele ya bunge la Kenya wiki hii kueleza zaidi kuhusu kukamatwa kwa Wakenya katika nchi jirani ya Uganda.

Wafugaji hao 8 kutoka Kenya wanahudumia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kushtakiwa na kukutwa na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria katika mahakama ya Kijeshi ya Uganda mwezi Aprili 2022.

Serikali ya Kenya inafanya jitihada za kuwaachilia wafungwa wa Kenya kupitia ushirikiano wa ngazi ya juu ya kidiplomasia. Picha Mtandao wa X, waziri Mutua 

Aidha, Aprili 8, mwaka huu, wachungaji 32 kutoka jamii ya Waturkana walikamtwa kwenye operesheni iliyofanywa na jeshi la Uganda la UPDF katika boma za wanyama za Waturkana, na kuhukumiwa katika mahakama ya kijeshi kwa kufungwa miaka 10 kila mmoja kwa kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria.

"Wafugaji wa Turkana walifikishwa katika mahakama ya kijeshi ndani ya siku moja bila kuruhusiwa uwakilishi wowote wa kisheria, haki ya kukata rufaa au haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria inayotoa haki ya kujitetea hadi itakapothibitishwa kosa," alisema Mbunge wa Loima, Protus Akujah katika maombi ya Bunge yaliyopelekea majibu ya Wizara.

Hata hivyo, Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameshikilia kuwa, mazungumzo yoyote kuhusu msamaha kwa Wakenya waliozuiliwa hayatokubalika hadi mauaji ya wanajiolojia 3 wa Uganda yatatuliwe au fidia itolewe kwa familia za wahasiriwa

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Kenya Kimani Ichungwa, ameiambia bunge kuwa Serikali ya Kenya inafanya jitihada za kuwaachilia wafungwa wa Kenya kupitia ushirikiano wa ngazi ya juu ya kidiplomasia.

“Suala hili limekuwa ngumu wakati Rais wa Uganda Yoweri Museveni alipotoa Amri ya Utendaji namba 3 ya 2023, iliyotolewa Mei 18, 2023, ambayo pamoja na mambo mengine, iliipa Kenya muda wa miezi sita kujibu suala la mauaji ya wanajiolojia, la sivyo, jamii ya Turkana hawataruhusiwa kulisha mifugo Uganda,” Ichung'wa alisema.

Hata hivyo serikali ya Kenya inasema kuwa inaendeleza mipango ya mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Dk. Alfred Mutua, Waziri wa Masuala ya Kigeni na mwenzake wa Uganda Gen. ODONGO Jeje Abubakhar.

TRT Afrika