Siku ya Mashujaa ni siku ya kitaifa nchini Kenya, ambayo huadhimishwa kila tarehe 20 mwezi Oktoba kama sikukuu ya kuwaenzi kwa pamoja wale wote waliochangia katika mapambano ya Kenya, uhuru au mchango chanya katika uhuru wa Kenya.
TRT Afrika iliongea na na baadhi ya Wakenya wa matabaka mbali mbali kuhusu maoni yao ya siku hiyo ya mashujaa.
Immaculate Wacera ambae ni mtaalamu ya masuala ya fedha anasema kuwa kwa miaka mingi shujaa wake alikuwa ni rais wa zamani wa Kenya Mwai Kibaki.
" Wakati huu ni vigumu kutaja shujaa wa sasa, zamani ilikuwa rahisi kusema mashujaa ni wale waliotupigania uhuru kama maumau, lakini siku hizi ni vigumu," Wacera anasema.
" Wakati wa miaka iliyopita ningesema kuwa rais wa zamani wa Kenya Mwai kibaki alikuwa shujaa wangu lakini sasa, naweza kusema mama yangu mzazi, kwani amenishikilia kabisa kimaisha, yeye ndiye shujaa wangu wa leo," Wacera anaongezea.
Naye Milka Kagea ambaye pia ni mkaazi wa Nairobi na anafanya kazi ya usaidizi nyumbani anasema kuwa kwake mashujaa wake ni wazazi wake kwani walimsaidia.
" Zamani ilikuwa rahisi kwetu kuongelea mashujaa kwani uchumi ulikuwa mzuri, lakini sasa uchumi ni mgumu na ni vigumu hata kuokota shilingi moja, hivyo huwezi kusema kuwa kiongozi yeyote ni shujaa wetu," Milka anasema.
Mkenya mwingine Jane Waigwa anasema shujaa wake ni mwajiri wake.
"Mashujaa wangu ni waajiri wangu wa sasa kwa sababu ndiyo wananisaidia kuweka chakula mezani," Waigwa anasema.
" Sijaifurahia sana siku hii ya leo kwa sababu kwa hali ya kawaida ningekuwa nyumbani nikipumzika na kusheherekea, lakini kwa sababu uchumi umekuwa mgumu lazima niede kazini leo ili niwapatie watoto wangu mlo wa leo."
Peter Wafula, ambaye ni dereva wa taksi anasema kuwa ni muhimu kubaki na uzalendo licha ya changamoto.
"Unaweza kuwa shujaa wako mwenyewe si lazima iwe viongozi wetu wa kisiasa, lazima tuanze kujiinua pia na kujipa moyo kuwa sisi ni shujaa pia," Wafula anasema.
Siku ya taifa ya mashujaa imesherehekewa na rais na viongozi wengine wa taifa katika mji wa Kericho.