Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Kumekuwa na mvutano kati ya Serikali ya Kenya na raia wa nchi hiyo kuhusu pendekezo la kuongezeka kwa ushuru katika sekta mbalimbali.
Bunge la taifa la nchi hiyo limejadili muswada huu huku sekta tofauti zikipinga pendekezo la ongezeko la ushuru.
Awali Serikali ilifanya mapendekezo hayo katika muswada wa fedha 2024 kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani ya nchi.
Hata hivyo, wadau mbalimbali nchini humo wamelalamika na kusema kuwa, mabadiliko hayo iwapo yatapitishwa, basi yataongeza gharama ya maisha kwa Wakenya.
Mamlaka ya Kutoza Ushuru ya Kenya KRA inalenga kukusanya KShs 2.768 Trilioni kufikia mwisho wa Mwaka wa Fedha wa 2023/2024 na kuvuka kiwango cha KShs 3 Trilioni kufikia Mwaka wa Fedha wa 2024/2025.
Hata hivyo, mapendekezo haya, yanaonekana kuligawa taifa, kwani, kuna wanaounga mkono na wanaopinga.
Je, wale wanaopinga wanasemaje?
Kuna pendekezo la kuongeza ushuru wa mazingira, ambapo Muungano wa Watengenezaji Betri za Magari unasema ni wazo bora lakini litamgharimu mwananchi zaidi pindi anaponunua betri ya gari yake.
Pendekezo la serikali ni kuongeza kodi ya mazingira kwa takriban dola 6 kwa kila kilo ya betri.
Betri ndogo ina wastani wa kilo 12 na iwapo kodi ya mazingira kwa betri hizi ndogo itaongezeka kwa takriban dola 69, hivyo basi, pamoja na VAT, mwananchi atanunua betri hii kwa dola 134 kutoka dola 65.
Kwenye betri ya kutumia nishati ya jua yenye uzito wa kil 60, kodi hii mpya itaongeza bei yake kwa dola 345. Taasisi za fedha pia zimelalamika kutokana na pendekezo la kuongeza ushuru kutoka 15% hadi 40% .
Zinadai kuwa muswada wa fedha 2024 utaongeza VAT kwenye huduma mbalimbali za kifedha ikiwa ni pamoja na kadi za benki, miamala ya pesa kwa njia ya simu, utunzaji wa fedha za kigeni na mengineyo.
Benki zinadai kuwa ada za huduma za kibenki si malipo ya moja kwa moja kwa chochote bali ni urejeshaji wa gharama wanayotumia kutoa huduma. Kuhusu miamala ya ubadilishanaji wa fedha za kigeni, ushuru unaopendekezwa wanasema utapanua wigo wa malipo ya ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Hii wanadai itachelewesha ukuaji wa uchumi kwa kutoza ushuru kwa mauzo ya nje na kuzuia ushindani wa bidhaa za Kenya.
Nao muungano wa watoa huduma za bima nchini Kenya umeliomba bunge kutopitisha pendekezo la kuongeza ushuru wa gari. Muswada wa sheria ya fedha umeleta ushuru wa magari uliowekwa wa 2.5% ya thamani ya gari ambayo inaweza kufika hadi dola 767.
Wataalamu wa bima wanasema hii itaongeza gharama ya bima ya magari. Kwa sasa, kiwango cha wastani cha malipo ya bima kinasimama kwa 5% na kwa ziada ya 2.5%.Kwa hivyo malipo ya bima sasa yatafikia 7.5%. Kwa upande wake, Chama cha watengenezaji mafuta ya kupikia nchini Kenya pia kimeibua wasiwasi kuhusu pendekezo la kuongezeka kwa tozo za ushuru.
Muswada mpya unapendekeza asilimia 25 ya ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya kupikia. Wanadai kuwa muswada huo ukipitishwa utachochea kuongezeka kwa mafuta ya kupikia ambayo ni hitaji muhimu kwa kila familia. Bei ya mafuta ya kupikia itaongezeka kwa asilimia 80.
Bidhaa zinazotengenezwa na mafuta ya kupikia nazo zitaongezeka bei, kama mkate, mandazi chapati na chips. Bei ya kawaida ya mkate wa 400gms itapanda kutoka shilingi 70 ya Kenya hadi 80 za sasa.
Zaidi ya hii, vifaa vyengine vinanyohusina na mafuta ya kupikia pia vitaongezeka bei. Kwa mfano bei ya sabuni inaweza kupanda kutoka 180 Kshs hadi 270 na siagi ya gramu 250 kutoka shillingi 160 hadi 300.
Sekta hii inaajiri zaidi ya watu 10,000 na kutoa ajira 30,000 ambazo sio za moja kwa moja.
Haya ni baadhi tu ya mapendekezo machache ya serikali ya kuongeza ushuru. Wananchi wanaendelea kupaza sauti wakisema serikali inawabana wakati ambapo tayari gharama ya maisha imepanda.
Wabunge wa Kenya hivi sasa wanaangaliwa kwa karibu, iwapo watasikiliza na kuzingatia kilio cha wananchi au la kabla ya kusomwa kwa bajeti ya nchi Juni 13, mwaka huu?