Uzalishaji wa pareto nchini umepungua kutoka kiwango cha juu cha tani 18,000 mwaka 1992 hadi uzalishaji wa sasa wa kitaifa wa takriban tani 500 kwa mwaka/ Picha: Msemaji wa serikali Kenya 

Katika miaka ya 1990, pareto ilikuwa zao la tatu kwa mauzo ya nje kwa Kenya, likitoa mapato kwa zaidi ya wakulima wadogo 200,000.

Wizara ya Kilimo inasema wakati huo, Kenya ilidhibiti zaidi ya asilimia 75 ya soko la pareto duniani. Leo, hisa ya Kenya ya soko imeshuka hadi asilimia mbili pekee.

"Serikali inaweka juhudi kubwa kufufua sekta hii muhimu. Kurahisishwa kwa soko, kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mazao kumefufua maslahi miongoni mwa wakulima na wawekezaji," msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema.

Serikali inawekeza katika kaunti ya Nakuru ikilenga kuimarisha ukuzaji wa pareto kwa kuhakikisha kuwa angalau ekari 30,000 za ardhi zimewekwa chini ya zao.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kaunti ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Leonard Bor alisema hii ni sehemu ya mkakati wa kufufua kikamilifu ukuaji wa pareto.

"Athari za kilimo cha pareto katika maisha ya wakazi wa Kaunti hii zimekuwa za ajabu. Huku wakulima wakizalisha wastani wa kilo 600 kwa ekari ya maua makavu kila mwezi, mapato ya wastani yanafikia dola za Marekani1,366. Hili limefikiwa kwa gharama ndogo za uzalishaji, jambo ambalo limefanya kilimo cha pareto kuwa uwekezaji wa kiuchumi,” alisema Bor.

Serikali imewekeza katika kiwanda cha Pareto katika kaunti ya Nakuru / Picha: Msemaji wa Serikali Kenya 

Pareto hukuzwa katika kaunti 18 nchini Kenya huku Nakuru, Nyandarua na Pokot Magharibi zikiwa wazalishaji wakuu wa zao hilo la biashara ambalo hapo awali lilibatizwa jina la ‘White gold of Kenya.’

Uzalishaji wa pareto nchini umepungua kutoka kiwango cha juu cha tani 18,000 mwaka 1992 hadi uzalishaji wa sasa wa kitaifa wa takriban tani 500 kwa mwaka.

'Pyrethrin' mara nyingi hutumiwa katika dawa za wadudu na bidhaa za nyumbani ili kudhibiti wadudu kwenye wanyama au mifugo. Pareto, dawa ya kuua wadudu, huathiri aina mbalimbali za wadudu katika bustani au mashamba.

Upandaji wa majaribio wa pareto nchini Kenya ulianza mnamo 1926 na tani chache za kwanza ziliuzwa nje miaka sita baadaye.

TRT Afrika