Kampuni ya habari ya kundi la The Standard ya nchini Kenya imetoa notisi ya kupunguza baadhi ya wafanyakazi wake.
" Notisi ya kupunguzwa kazi itaanza kutumika baada ya kuisha kwa tangazo la mwezi mmoja lililotolewa tarehe 31 Julai 2024 na linatarajiwa kuathiri zaidi ya wafanyakazi 300 katika idara mbalimbali," ilisomeka notisi hiyo.
" Wafanyakazi wote walioathirika watafahamishwa kwa maandishi," imesema notisi hiyo.
Kampuni hiyo imesema wafanyakazi watakaoathiriwa watalipwa kwa siku walizohudumu kazini kabla ya kusimamishwa.
Kampuni ya The Standard Group inamiliki vyombo kadhaa vya habari vikiwemo, gazeti la The Standard, televisheni za KTN na KTN News, Radio Maisha na vitengo vingine vya kidijitali.
Kampuni hiyo inataka kutengeneza upya biashara ili iwe " na watu wachache na muundo bora zaidi kwa utendaji bora na ukuaji."
Imetoa notisi ya kuwafidia wafanyakazi kulingana na mikataba yao na siku zao za mapumziko kabla ya kuacha kazi.
Waathrika wa maamuzi hayo, pia watalipwa malipo ya uzeeni kulingana na sheria za mfumo wa malipo hayo.
Kampuni ya kundi la The Standard, ilianzishwa mwaka 1902 ikiwa kampuni ya kwanza kuwekeza katika mifumo tofauti ya habari, ikiwa na vitengo vya magazeti, televisheni, redio kidijiti.
Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels