Juhudi zimeshika kasi kwa Afrika Mashariki kuandaa kombe la taifa bingwa Afrika mwaka 2027.
Katika mradi walioupa jina la ‘Pamoja,’ - Kenya, Uganda na Tanzania wanataka kuandaa kombe hilo kubwa zaidi barani kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe hilo.
Chachu ya kuandaa mashindano hayo ilizuka 2019, baada ya nchi nne za Afrika Mashariki kufuzu, kwa pamoja, ikiwa ndio mara ya kwanza kabisa katika historia ya kombe hilo kwa Afrika Mashariki kuwa na wakilishi wengi.
Sasa nchi hizi zimekuwa katika mashauriano kutafuta njia ya kuleta kombe hilo katika eneo lao.
Rais wa Kenya, William Ruto alielezea matumaini kuwa kuandaa kombe hilo kutafaidi zaidi mataifa yao.
‘Matumaini yetu ni kuwa kuandaa kombe hili kwa pamoja, kutawapa timu zetu za taifa motisha, sio kufuzu tu, bali kufanya vyema katika mchuano huo kupitia walivyofanya awali,’’ aliongeza rais Ruto.
Jumatatu, Waziri wa Michezo wa Kenya aliwasilisha kwa rais wakandarasi walioandaa upande wa Kenya ikiwa tayari kuwasilishwa kwa shirikisho la soka Afrika Caf, linalo kutana na kuchagua nchi itakayoandaa kombe hilo.
Upande wa Tanzania nao wamekuwa katika mikutano ya hali ya juu, ikiwemo kuwashirikisha Waziri wa Michezo na wadau wengine katika soka, ili kupanga mikakati ya namna watawasilisha ombi lao wakiwa pamoja na majirani, Kenya na Uganda.
Magwiji wa michezo wanategemea maandalizi ya kombe hili yatafaidi soka ya Afrika Mashariki kwa kuwaleta pamoja wachezaji na mashabiki kwa kutambulishana na kudumisha uhusiano wa kimpira kwani sasa kila mmoja anafuatilia tu ligi za nyumbani.
Saleh Jembe, Mchambuzi wa michezo Tanzania anasema, ‘Ukanda wetu bado ni dhaifu katika soka, ukilinganisha na Afrika Magharibi au Kaskazini. Hii itasaidia sana kuongeza uwekezaji na kuinua viwango vya viwanja vyetu na ufadhaili wa timu, na hivyo kukuza soka zaidi Afrika Mashariki.’’
Ameongeza kuwa, ‘Maandalizi haya yatawatambulisha wachezaji wetu nje ya eneo, na kuwezesha kutafutwa na kununuliwa kuchezea vilabu vikubwa ndani na nje ya Afrika.’’
Tarehe 23 Mei ndio siku ya mwisho kwa nchi zote kuwasilisha ombi lao la kuandaa kombe hilo. Wengine wanao wania fursa hiyo ni Algeria, ambao ndio waandaaji wa kombe la Afcon U17 mwaka huu, Botswana na Misri.
Hata hivyo nchi hizi zitalazimika kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya soka kinyumbani ikiwemo kuimarisha viwanja vyao, kuweka sawa usimamizi wa mashirikisho yao ya soka na kuimarisha usalama wa kitaifa ili kuwawezesha kuandaa shindano hilo la kimataifa.
Miongoni mwa masharti yaliyopo ni kuwa viwanja visiwe mbali na uwanja wa ndege, mahoteli makubwa na hospitali kubwa zaidi nchini humo.
Kwa sasa, Tanzania pekee ndio ina uwanja unaotazamiwa kuweza kuandaa kombe hili, lakini itahitaji viwanja zaidi. Ndio maana itakuwa rahisi zaidi kwa nchi hizi kuandaa kwa pamoja.