Kenya inatumai uhusiano mwema kati yake na Uganda utaimarisha udugu wa mataifa ya Afrika Mashariki / Picha: Rais William Ruto

Viongozi wa Kenya na Uganda wametoa tangazo la kutafutia suluhu mvutano uliokuweopo kati yao juu ya usafirishaji wa mafuta kutoka bandari ya Mombasa, hadi nchi hiyo isiyokuwa na bandari.

Katika ukurasa wake wa X, zamani twitter, Rais WIlliam Ruto wa Kenya alielezea mkutano uliozaa matunda kati yake na mwenyeji wake Yoweri Museveni wa Uganda ambao uliangazia mgogoro wa uuzaji na usafirishaji mafuta ya Uganda kutoka Kenya.

''Nina furaha kwamba masuala yanayoathiri mtiririko wa bidhaa za petroli kati ya Kenya na Uganda yanatatuliwa,'' ilisema taarifa ya Rais Ruto. ''Tumekubaliana juu ya njia ya mbele ya kupata na kuratibu uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa kanda kwa namna ambayo itahakikisha tunapata bei ya ushindani zaidi na ufanisi wa juu zaidi wa vifaa,'' iliendelea kusema taarifa hiyo.

Kenya na Uganda zimekuwa na mzozo baada ya Nairobi kuikatalia Kampuni ya mafuta ya kitaifa ya Uganda UNOC, leseni ya kufanya kazi ndani ya nchi na kushughulikia uagizaji wa mafuta katika mji mkuu wa Kampala.

Masharti magumu ya Kenya

Kampuni hiyo ya UNOC ilitaka kufanya biashara hiyo kwa kutumia miundo mbinu ya Shirika la kitaifa la mafuta nchini Kenya KPC, na kuendesha shughuli zake kama biashara huru ya kigeni.

Kenya kwa upande wake ilitoa masharti mengi kabla ya hilo kukubalika ikiwemo kuitaka kampuni ya Uganda kujisajili kama muuzaji mafuta na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli ya Kenya (EPRA) ili kuiruhusu kuagiza na kuuza nje bidhaa za petroli kupitia Kenya kwa kutumia bomba la nchi hiyo.

EPRA iliomba UNOC itoe vyeti vya usajili wa biashara; hati za utambulisho kwa wakurugenzi wote; vibali vya kufanya kazi; vyeti vya kufuata kodi; uthibitisho wa uwezo wa kifedha ikiwa ni pamoja na uthibitisho wa mauzo ya lita milioni 6.6 za petroli ya juu au mafuta ya petroli au A1jet au mafuta ya taa nchini Kenya; ushahidi wa kuendesha vituo vitano vya rejareja vilivyoidhinishwa na bohari yenye leseni yenye mauzo ya dola milioni 10 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kutokana na masharti haya ya Kenya, Uganda iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki iliyo na makao yake mjini Arusha Tanzania, ikilalamikia kile ilichoona kama njama ya Kenya kuhujumu ukuaji wake wa sekta ya mafuta.

UNOC ilisisitiza kuwa ni kampuni rasmi ya serikali ambayo ilikuwa na nia ya kusafirisha bidhaa zake kupitia Kenya wala haikuwa na nia ya kufanya biashara ndani ya Kenya.

Pia mvutano huu kati ya Kenya na Uganda ulisababisha Uganda kutafuta njia mbadala ya kusafirisha mafuta kupitia bandari ya Tanga ya Tanzania.

Tanzania kwa upande wake imekuwa ikiendela na miradi yake ya kusasisha na kupanua bandari zake za Tanga na Bagamoyo, huku ikilenga biashara hiyo ya usafirishaji mafuta na bidhaa nyengine kwa nchi zisizo na bandari, kutumia miundo mbinu zake.

Mradi wa Mombasa- Eldoret- Kampala- Kigali

Rais Willam Ruto ameelezea matumaini kuwa kutatuliwa kwa mgogoro huu wa kibiashara kati yao kunaendana na azma ya kukuza udugu mwema kati ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

''Uhusiano huu ni pamoja na kuleta mataifa yote saba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki karibu katika lengo lao kuu la kuunda Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki,'' alisema Rais Ruto.

Pia viongozi hao wawili walijadiliana kurejelea mradi wa usanifu na ujenzi wa bomba la bidhaa iliyosafishwa ya mafuta ya petroli kupitia miji ya Eldoret-Kampala-Kigali.

Mradi huo wenye urefu wa kilomita 1800, ulikuwa unanuiwa kuunganisha hadi nchi nne, kuanzia bandari ya Mombasa - Kampala- Kigali na hatimaye Bujumbura kwa gharama ya dola bilioni 5.

TRT Afrika